Tahadhari kuhusu uwezekano wa kusambaratika usitishaji vita nchini Yemen
Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kuanzishwa tena operesheni za kijeshi, akiashiria ukiukaji vita wa mara kwa mara unaofanywa na muungano wa kijeshi wa Saudia.
Tangu tarehe 26 Machi 2015, wananchi wa Yemen wamekuwa wakishuhudia vita vya muungano wa kijeshi wa Saudia dhidi ya nchi yao. Vita hivyo vinavyoungwa mkono na Marekani na nchi za Ulaya, vimeua moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja watu zaidi ya 100,000 , kujeruhi mamia kwa maelfu, na kusababisha watu wapatao milioni 4 kuyahama makazi yao. Aidha, zaidi ya asilimia 85 ya miundombinu ya Yemen imeharibiwa kabisa au kuharibiwa sehemu kubwa kutokana na vita hivyo. Yemen ni nchi maskini zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu iliyo katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati).
Katika kipindi cha miaka 7 iliyopita, Umoja wa Mataifa na baadhi ya nchi za eneo zimefanya juhudi za kusimamisha vita huko Yemen, lakini uvurugaji mambo unaofanywa na watawala wa Aal Saud na ukosefu wa dhamira ya dhati kwa madola ya Magharibi ndio sababu ya kushindwa kuzaa matunda juhudi hizo. Mwishoni mwa mwaka wa saba wa vita, Wasaudi na Wayemen, kupitia mpango na upatanishi wa Umoja wa Mataifa, walikubaliana kuanzisha usitishaji vita wa miezi miwili, na usitishaji huo wa mapigano ulianza kutekelezwa mwezi Aprili na kurefushwa kwa miezi miwili zaidi mwezi Juni.

Kulikuwa na sababu moja kuu iliyowapelekea watawala wa Saudia kukubali kusitisha mapigano katika kipindi hicho. Sababu hiyo ilihusiana na matukio ya uwanja wa vita ambapo Wayemeni waliweza kuwasababishia mapigo makubwa Wasaudi na Saudia ikapata hasara nyingi, ikiwa ni pamoja na kuanikwa wazi udhaifu wa nchi hiyo ya kifalme.
Pamoja na hayo, watawala wa Aal Saud wamekuwa wakikiuka mara kwa mara usitishaji mapigano kati ya pande mbili. Hata kama katika kipindi cha miezi 3 iliyopita meli kadhaa zilizobeba bidhaa za mafuta na misaada ya kibinadamu zimewasili Yemen na vile vile uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a na Bandari ya Hudeidah kufunguliwa tena, lakini suala hilo halikuwafurahisha watawala wa Riyadh, ambao wamekuwa wakikiuka mara kwa mara mapatano ya usitishaji vita kwa kusimamisha meli zinazobeba mafuta kwenda Yemen na wakati huo huo kuvuruga safari za ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a pamoja na kufunga baadhi ya barabara muhimu nchini humo.
Mbinu hiyo inaonyesha wazi kuwa watawala wa Aal Saud wanataka usitishaji vita usio kamili nchini Yemen. Lengo la Aal Saud ni kuzuia kuendelea kwa mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Yemen dhidi ya Saudi Arabia kupitia usitishaji vita huo usio kamili. Kwa hakika kupitia mbinu hiyo utawala wa Riyadh unajaribu kuonyesha kwamba bado unadhibiti mwenendo wa vita huko Yemen na wakati huo huo kupunguza mashinikizo ya fikra za waliowengi duniani dhidi yake.
Katika mazingira hayo, baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, mienendo ya kutiliwa shaka ya Wasaudi katika Baraza la Uongozi la Yemen, lililochukua uongozi wa serikali iliyojiuzulu baada ya kuondolewa madarakani rais mtoro wa Yemen, Abd Rabbu Mansour Hadi, inaonyesha kwamba Saudi Arabia inataka kufufua nguvu zake na kuunda muungano mpya huko Yemen dhidi ya kundi la Ansarullah.

Mbinu hiyo, hata hivyo, imekabiliwa na ukosoaji, maandamano na onyo kali kutoka kwa Wayemen. Kuhusiana na suala hilo, Mahdi al-Mashat, Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen huku akisisitiza juu ya ulazima wa kuheshimiwa usitishaji vita, ametangaza upinzani wa Riyadh dhidi ya mapendekezo ya kufunguliwa upya barabara, kutosimamishwa meli zinazobeba mafuta na bidhaa za matumizi ya msingi na kuondolewa mzingiro dhidi ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana'a na Bandari ya Hudeidah. Kufuatia hali hiyo, Mahdi al-Mashat ameonya kuwa iwapo mbinu hiyo ya Aal Saud ya kukiuka mara kwa mara usitishaji vita itaendelea, kila kitu kinaweza kubadilika na kuanzishwa tena operesheni za kijeshi dhidi ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na utawala huo wa kifalme nchini Yemen.
Hussein al-Azi, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen pia ameutahadharisha muungano huo wa Saudia katika ujumbe wake wa Twitter kwamba iwapo hakutafikiwa mapatano ya kuaminika, mapana, ya kutegemewa na athirifu na ambayo yanajumuisha nyanja zote za kibinadamu na kiuchumi, ikiwa ni pamoja na mapato ya mafuta na gesi, hapatakuwa tena na nafasi ya kurefushwa usitishaji vita wa hadaa na uwongo katika uwanja huo.