UN na jitihada za kuongeza muda wa usitishaji vita huko Yemen
Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, umoja huo unafanya juhudi ili kuongeza muda wa usitishaji vita huko Yemen.
Makubaliano ya usitishaji vita yaliyofikiwa huko Sweden na ujumbe kutoka Sana'a na ule wa Riyadh yalianza kutekelezwa tangu Jumanne asubuhi Disemba 18, 2018 katika baadhi ya mikoa ya Yemen, hata hivyo muungano vamizi nchini humo chini ya uongozi wa Saudi Arabia kila siku unakiuka makubaliano hayo.
Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, Farhan Haq Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, Hans Grundberg Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa Katika Masuala ya Yemen amekuwa akiwasiliana na pande za Yemen huku akijaribu kila linalowezekana kuongeza muda wa usitishaji vita nchini humo.
Hans Grundberg jana Jumatatu alieleza kuwa, makubaliano ya usitishaji vita huko Yemen yamepelekea kupungua sana mauaji ya raia kiasi kwamba vifo vya raia vimepungua kwa theluthi mbili ikilinganishwa na miezi mitatu kabla ya kuanza usitishaji vita.
Hii ni katika hali ambayo, Abdulwahab Yahya al Dara Waziri wa Usafirishaji wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen jana pia alieleza kuwa, usitishaji vita nchini humo zaidi umekuwa ukitumika kwa ajili ya kuiba mafuta ya Yemen na kusisitiza kuwa: haina maana yoyote kuongeza muda wa usitishaji vita bila ya kupanua wigo wake na kunapasa kufanyika marekebisho katika vipengee vya usitishaji vita huo na pande za muungano vamizi wa Saudia na Imarati.
Itafahamika kuwa, duru ya pili ya usitishaji vita kwa ajili ya masuala ya kibinadamu chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa inakaribia kumalizika; ambapo duru hiyo haijatekelezwa kikamilifu hadi sasa pasina na wananchi wa Yemen kupunguziwa makali na masaibu yanayowakabili. Bali usitishaji vita huo umeuandalia muungano vamizi mazingira mazuri na salama ya kuendelea kupora na kuuza nje mafuta ya Yemen.