Sana'a: Fedha ya Imarati na Saudia haiwezi kutupigisha magoti
Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, fedha ya Imarati na Saudi Arabia imeipigisha magoti sehemu kubwa ya hii dunia, lakini haiwezi kuiburuta na kuipigisha magoti serikali ya Sana'a.
Abdul Aziz Saleh bin Habtoor Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen amesema kuwa, wananchi wa Yemen wamekuwa wakitekeleza kila wawezalo ili kuilinda nchi yao.
Bin Habtoor ameongeza kuwa, hakuna nchi iliyofikiria kwamba taifa la Yemen pamoja na suhula chache ilizonazo lingeweza kuendesha muqawama na kukabiliana na muungano vamizi uliojizatiti kwa silaha na zana zote ulizopatiwa na Imarati na Saudia.
Miaka minane imepita sasa Yemen inaendelea kuwa ngangari na kusima kidete mbele ya uvamizi wa Saudia na washirika wake kwa hiyo fedha za Imarati nan Saudia ambazo zimeipigisha magoti sehemu kubwa ya dunia hii kamwe haziwezi kuipigisha magoti Sana'a.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokovu wa kitaifa ya Yemen amesema, inashangaza kuona suala la kusitisha vita Yemen na kuongeza muda wake limejadiliwa na nchi vamizi na waungaji wao mkono katika kikao cha Jeddah.
"Kama kweli kuna yoyote mwenye nia ya kweli ya kusitisha vita huko Yemen au kurejesha amani nchini humo basi anapasa kufuatilia suala hilo huko Sana'a. Sisi tunajifakharisha kuwa sehemu ya muqawama, na hatuutambui rasmi utawala ghasibu wa Israel," amesema Abdul Aziz bin Habtoor.
Katika upande mwingine, Muhammad Abdulsalaam Msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen jana usiku alieleza kuwa, muungano vamizi unaoongozwa na Saudia hautekeleza kikamilifu mapatano ya kusitisha vita na unatumia kipropaganda suala la kufunguliwa tena njia na barabara mbalimbali huko Yemen.