Hamas: Wazayuni hawatafaulu kamwe kuiyahudisha Quds tukufu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i86166-hamas_wazayuni_hawatafaulu_kamwe_kuiyahudisha_quds_tukufu
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, amri ya kuharibiwa nyumba za Wapalestina na kuwazuia kujenga huko Quds tukufu (Jerusalem) kamwe haitaweza kuharibu makumbusho na athari zake za kihistoria na Kiislamu za eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 22, 2022 08:39 UTC
  • Hamas: Wazayuni hawatafaulu kamwe kuiyahudisha Quds tukufu

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, amri ya kuharibiwa nyumba za Wapalestina na kuwazuia kujenga huko Quds tukufu (Jerusalem) kamwe haitaweza kuharibu makumbusho na athari zake za kihistoria na Kiislamu za eneo hilo.

Muhammad Hamadeh, Msemaji wa Hamas amesema mapema leo Ijumaa kwamba, hatua ya utawala ghasibu wa Israel ya kutoa makumi ya amri za kuharibu na kuzuia ujenzi wa nyumba na taasisi za kiraia katika mji wa Quds inayokaliwa kwa mabavu ni jinai mpya ya Wazayuni na vita vya wazi dhidi ya kuwepo Wapalestina katika mji huo mtakatifu.

Hamadeh amefafanua kuwa, utawala ghasibu wa Israel hautafanikiwa kamwe kuwafanya Wapalestina wasalimu amri na kuharibu makumbusho ya kihistoria ya Quds.

Msemaji wa Hamas amesisitiza kuwa, mji wa Quds ni ardhi ya Wapalestina, na wavamizi hawana mamlaka yoyote katika eneo hilo. Amesema taifa lenye msimamo thabiti na madhubuti la Palestina litaendelea kuwa na msimamo imara katika ardhi yake na litakabiliana ipasavyo na vita hivyo vya Wazayuni kwa uwezo wake wote licha ya jitihada zinaofanywa na Marekani za kujaribu kufunika na kukahalalisha jinai na uhalifu mkubwa wa wavamizi hao, ambazo zimeonekana waziwazi katika taarifa ya karibuni ya Rais Joe Biden wa Marekani na waziri mkuu wa Israel.

Biden akiwa safarini Tel Aviv

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa wakati wa safari ya Joe Biden huko Tel Aviv, Marekani iliahidi tena kulinda usalama wa utawala haramu na ghasibu wa Israel na kuhakikisha kwamba unakuwa na nguvu kubwa zaidi ya kijeshi katika eneo la Magharibi mwa Asia. 

Kwa kubomoa nyumba za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi yao, utawala wa Israel unajaribu kubadilisha muundo wa kijiografia na wa idadi ya watu wa maeneo ya Palestina na kuyapa nembo na alama za Kizayuni na Kiyahudi.