Umoja wa Mataifa walaani milipuko mtawalia nchini Afghanistan
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake mkubwa kufuatia mfululizo wa milipuko inayotokea nchini Afghanistan ambayo imeua na kujeruhi zaidi ya watu 250 mwezi huu wa Agosti, ikiwa ni pamoja na watoto.
Kwa mujibu wa msemaji wa Antonio Guterres, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali shambulio la hivi liliowalenga waumini waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya Swala katika msikiti mmoja ulioko Khair Khana, viungani mwa Kabul.
“Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga na kuwatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa.
Vitendo vyovyote vya kigaidi ni vya jinai na havikubaliki, bila kujali sababu zao, popote walipo, wakati wowote na yeyote aliyetenda.” Imeeleza taarifa hiyo na kusisitiza kuwa, Waafghan wote wana haki ya kuishi kwa amani na kutumia uhuru wao wa dini.
Jana msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amelaani shambulio la kigaidi lililopelekea kuuawa makumi ya watu katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Nasser Kanaani, alilaani hujuma hiyo iliyolenga waumini waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya Swala katika msikiti mmoja ulioko Khair Khana, viungani mwa Kabul.
Amesema: Iran inatoa mkono wa pole kwa wananchi na serikali ya Afghanistan kutokana na shambulio hilo la kikatili lililofanywa na magaidi wasio na chembe ya utu.
Hadi sasa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi hilo lakini weledi wa mambo wanaamini kuwa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh ndilo lililohusika.
Mapema mwezi huu, kundi hilo la kigaidi lilikiri kuhusika na mlipuko mwingine uliotokea huko Kabul, mji mkuu wa Afghanistan, ambao ulipelekea watu 8 kuuawa shahidi na wengine 18 kujeruhiwa.