Balozi wa UAE kurejea Iran kuimarisha zaidi uhusiano
Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini Iran, Saif Mohammed Al Zaabi, ataanza tena kazi yake mjini Tehran katika siku zijazo ikiwa ni katika juhudi za kuimarisha uhusiano wa pande zote.
Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE imesema uamuzi huo ulifanywa "kuambatana na juhudi za UAE za kuimarisha uhusiano na Iran na kama sehemu ya uamuzi wa hapo awali wa kuinua uwakilishi wa kidiplomasia hadi cheo cha balozi."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, hatua hiyo imekuja kufuatia mazungumzo ya simu ya hivi majuzi kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa UAE Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan.
Hali kadhalika taarifa hiyo imebainisha kuwa Al Zaabi ataanza tena majukumu yake katika ubalozi wa UAE mjini Tehran kwa uratibu na Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran "kulingana na kanuni za kidiplomasia zinazosimamia uhusiano wa pande mbili."
Kulingana na wizara hiyo, hatua hiyo inalenga "kufikia maslahi ya pamoja ya nchi hizo mbili na eneo kubwa zaidi."
Katika miezi ya hivi karibuni, Iran na UAE zimezidisha juhudi za kujenga upya uhusiano ulioathiriwa na vita vya miaka mingi nchini Yemen na masuala mengine ya kikanda.
UAE ambayo ni kitovu cha biashara katika Ghuba ya Uajemi imekuwa muuzaji mkuu wa bidhaa na mashine kwa Iran tangu 2018 wakati Tehran ilipowekwa chini ya msururu wa vikwazo vya kiuchumi vya upande mmoja na Marekani.
Thamani ya mauzo ya nje ya UAE kuja Iran inafikia zaidi ya dola bilioni 1.5 kwa mwezi, kulingana na takwimu za ofisi ya forodha ya Iran.
Katika ujumbe kwa Rais wa UAE Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan mwezi Mei, Rais Ebrahim Raeisi wa Iran alitumai kuwa Tehran na Abu Dhabi zingeboresha zaidi uhusiano katika nyanja zote ili kuhudumia maslahi ya pamoja.
Mapema mwezi huu, Kuwait nayo pia ilimteua Bader Abdullah al-Munaikh kuwa balozi wake nchini Iran, zaidi ya miaka sita baada ya nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi kumuita tena mjumbe wake kutoka Tehran kufuatia uamuzi wa Saudi Arabia wa kukata uhusiano wa kidiplomasia na Jamhuri ya Kiislamu.
Kuwait ilipunguza uhusiano wa kidiplomasia na Iran hadi kiwango cha balozi mdogo Januari 2016.
Hayo yalijiri kufuatia uamuzi wa Saudi Arabia kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran mnamo Januari 2016 baada ya waandamanaji wa Iran, waliokasirishwa na mauaji ya Saudia dhidi ya kiongozi mashuhuri wa Kishia Sheikh Nimr Baqir al-Nimr, kuvamia ubalozi wake mjini Tehran.
Kuimarika uhusiano wa Iran na Kuwait na UAE kunakuja huku kukiwa na juhudi pana za Tehran na Riyadh za kupunguza na kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia.