Makubaliano rasmi yafikiwa Iraq katika muungano wa "Uundaji wa Serikali"
Sep 26, 2022 07:30 UTC
Mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Vuguvugu la Hekima ya Kitaifa la Iraq ametangaza kuwa makubaliano rasmi yamefikiwa kati ya Masunni, Mashia na Wakurdi juu ya kuunda muungano unaojulikana kama "Uundaji wa Serikali".
Kwa mujibu wa Al-Sumaria News, Fadi Al-Shammari, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Vuguvugu la Hekima ya Kitaifa la Iraq, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: "makubaliano rasmi ya kuunda muungano wa "Uundaji wa Serikali", yametiwa saini na vyama vya muungano huo unaojumuisha Mfumo wa Uratibu, Chama cha Kidemokrasia cha Kurdistan, Muungano wa Kitaifa wa Kurdistan, Muungano wa Al-Siyadah, Babylon na Muungano wa Azma.
Kwa mujibu wa kipengele kimojawapo cha makubaliano ya muungano wa Uundaji wa Serikali, mgombea wa muungano huo kwa ajili ya nafasi ya uwaziri mkuu wa Iraq ni Mohammed Shiyaa Al-Sudani.
Wanachama wa muungano wa Uundaji wa Serikali wamekubaliana pia juu ya kutofanya mazungumzo yoyote na Harakati ya Sadr kwa sababu harakati hiyo imelikataa pendekezo la kufanya mazungumzo.
Muungano huo umeainisha tarehe 27 Septemba kuwa ndio siku ya kuanza tena shughuli za bunge la Iraq na kubainisha pia kwamba sheria ya uchaguzi itaandikwa upya na uchaguzi utafanyika mwaka mmoja baada ya hapo.
Uchaguzi wa mapema wa bunge la Iraq ulifanyika Oktoba 10, 2021, lakini licha ya kupita miezi 11 tangu ulipofanyika uchaguzi huo, hadi sasa makundi, vyama vya siasa pamoja na mirengo iliyoko bungeni haijaweza kuunda serikali mpya kutokana na tofauti za kisiasa zilizoko baina yao.../