Usitishaji usiositishwa wa vita vya Yemen
Sambamba na kukaribia tarehe Pili Oktoba, siku utakapokamilika muhula wa miezi miwili wa usitishaji vita nchini Yemen, zoezi la kusimamisha mapigano katika vita vya nchi hiyo ambalo lilianza rasmi tarehe Pili Juni mwaka huu, litakuwa limekamilisha duru yake ya pili.
Hii inamaanisha kwamba, tokea hapo awali, lengo na sababu ya Marekani kuunga mkono usitishaji vita huko Yemen haikuwa ni kuguswa na hali mbaya ya kibinadamu, wala kufanikisha upelekaji huduma na misaada nchini humo; bali ni kuhakikisha vituo vya mafuta vya Saudi Arabia vinasalimika na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za vikosi vya ulinzi vya Yemen. Kwa sababu, kama msimamo wa Washington ungekuwa umetokana na sababu za kiutu, ingefuatilia usitishaji vita nchini Yemen kabla mtikisiko wa vita vya Ukraine haujateteresha masoko ya nishati na matumizi yake katika nchi za Magharibi. Na baada ya hapo, ingeishinikiza pia Saudi Arabia ikomeshe mwenendo wake wa kukiuka mara kwa mara usitishaji vita huo. Lakini baada ya kusitishwa mapigano, Marekani iliondoa mashinikizo iliyokuwa imeiwekea Saudia, ili kwa upande mmoja, kuifanya ihalifu bila ya hofu ahadi ilizowekeana na Russia katika jumuiya ya OPEC+; na kwa upande mwingine, kupata njia pia ya kuilazimisha iongeze uzalishaji wake wa mafuta; na mkabala wake, Riyadh nayo kupata ujasiri na uthubutu wa kuendelea kutekeleza bila hofu malengo ya kijeshi inayofuatilia nchini Yemen.
Kujitokeza na kuendelea kwa hali hii kumeifanya serikali na wananchi wa Yemen wawe na shaka na hatihati ya kurefusha tena usitishaji vita; kwa sababu kiuhalisia, hawajaona mabadiliko yoyote katika mwenendo na muamala wa madola vamizi; na mkabala wake, kutokana na wao kufungika mikono kwa kisingizio cha usitishaji vita, hawawezi kufanya chochote ili kujibu uchokozi na ukiukaji wa mara kwa mara wa usitishaji mapigano unaofanywa na madola hayo. Na ndiyo kusema kuwa, usitishaji huo wa mapigano ama umeyanufaisha madola vamizi kwa kuweza kuimarisha kuwepo kwao kijeshi katika maeneo ya Yemen yanayoyakalia kwa mabavu; au umeyanufaisha madola ya Magharibi, ambayo yamefanikiwa kuzuia kupanda tena bei ya nishati, na vilevile kwa kuyatumia madola vamizi ya Saudia na Imarati pamoja na vibaraka wao, yanaweza kununua kwa bei rahisi rasilimali za mafuta na gesi ya Yemen zinazoporwa na makampuni ya mafuta na gesi ya nchi hizo.
Kwa kuzingatia kuwa ndege zote zilizotumiwa katika mashambulio hayo zimetengenezwa Marekani au Ulaya, kwa hivyo serikali za Magharibi nazo pia zinahusika na zimeshiriki katika jinai za kivita zilizofanywa na majeshi vamizi ya Saudia na Imarati. Katika muda wa miezi minne ya usitishaji vita, Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen imetoa fursa kwa madola vamizi na waungaji mkono wao wa Magharibi kurekebisha mtazamo wao, lakini kwa kuzingatia kwamba hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa na madola hayo, sasa imeamua kwa mara nyingine tena kupigania haki yake ya kujihami.../