Watoto 11 wawa wahanga wa mashambulio ya Marekani Syria
Kundi linalojiita la haki za binadamu nchini Syria limesema kuwa, mashambulizi ya muungano unaodaiwa ni wa kupambana na Daesh yameua raia wasiopungua 30 wakiwemo watoto wadogo 11.
Ripoti ya kundi hilo imesema kuwa, muungano huo unaoongozwa na Marekani jana ulifanya mashambulizi katika mji wa Manbij ulioko umbali wa kilomita 446 kaskazini mwa mji mkuu wa Syria, Damascua. Kundi hilo la haki za binadamu lenye makao yake mjini London Uingereza limesema kuwa, watoto wadogo 11 ni miongoni mwa wahanga wa mashambulizi hayo. Ripoti hiyo imekuja ikiwa imepita zaidi ya wiki moja tangu raia wasiopungua 15 wakiwemo watoto wadogo watatu kuuawa katika mashambulizi ya Marekani dhidi ya eneo lililodhaniwa ni la wanamgambo wa ISIS mjini humo. Watu 10 wa familia moja walipoteza maisha yao tarehe 21 mwezi uliopita wa Mei wakati muungano huo unaodaiwa ni wa kupambana na Daesh uliposhambulia kijiji cha Arshaf kilichoko umbali wa kilomita nane kutoka katika mji wa Marea. Ikumbukwe kuwa tangu mwezi Septemba 2014 muungano unaoongozwa na Marekani umekuwa ukifanya mashambulizi ya anga ya eti kupambana na magaidi wa Daesh bila ya idhini ya serikali ya Syria na wala ruhusa ya Umoja wa Mataifa. Mara kwa mara muungano huo umekuwa ukilaumiwa kwa kuua watu wasio na hatia. Cha kushangaza ni kuwa mashambulizi ya muungano huo hayaoneshi dalili zozote za kulidhoofisha kundi la kigaidi la Daesh.