Majeshi ya Syria yazidi kupata ushindi Latakia
Jeshi la Syria likisaidiwa na wananchi limefanikiwa kuwatimua wapiganaji wa makundi ya kigaidi katika vijiji vinne muhimu katika eneo la Latakia karibu na mpaka wa nchi hiyo na Uturuki.
Duru za habari zinaripoti kuwa, jeshi la Syria limefanikiwa kudhibiti vijiji vya al-Hoor, al-Rweisat, al-Sweidia na al-Wadiil-Azraq bila upinzani mkubwa. Shirika la habari la SANA la nchini Syria limeripoti kwamba idadi kubwa ya magaidi wameuawa na wengine wamekimbilia kwenye maeneo ya mpakani. Kufuatia ushindi huo, jeshi la Syria sasa linakaribia ngome ya mwisho ya magaidi ambayo ni Kinsabba katika mkoa huo wa Latakia. Mafanikio kama hayo pia yameshuhudiwa katika maeneo ya Homs na Aleppo.
Tangu kuanza mgogoro wa Syria miaka 5 iliyopita, watu wasiopungua laki mbili wamepoteza maisha na zaidi ya nusu ya idadi jumla ya watu katika taifa hilo wamekimbia makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za nje.
Serikali ya Damascus imesisitiza kuwa itapata ushindi dhidi ya magaidi na waungaji mkono wao Mashariki ya Kati na katika nchi za Magharibi.