Takwimu za kutisha kuhusu hukumu za kunyonga watu nchini Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i89194-takwimu_za_kutisha_kuhusu_hukumu_za_kunyonga_watu_nchini_saudia
Takwimu zilizotolewa na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu zinaonyesha kuwa Saudi Arabia imewanyonga watu 1,100 katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 12, 2022 08:31 UTC
  • Takwimu za kutisha kuhusu  hukumu za kunyonga watu nchini Saudia

Takwimu zilizotolewa na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu zinaonyesha kuwa Saudi Arabia imewanyonga watu 1,100 katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Utawala wa Aal Saud aidha unaongoza katika orodha ya nchi zinazonyonga watu kwa wingi; ambapo utawala huo mara nyingi umekuwa ukitoa hukumu ya kunyongwa kwa wanaharakati, wanazuoni wa kidini, wapinzani wa serikali na watetezi wa haki za binadamu ambao hujumuisha wanaume, wanawake na hata wale walio chini ya umri wa kisheria. Hii ni katika hal ambayo, watu hao hunyongwa kwa siri na kinyume na sheria za Kiislamu na kimataifa.    

Utawala wa Aal Saud na kukithiri hukumu za kunyonga watu 

Serikali ya Saudi Arabia kila mwaka huwakuhumu kunyongwa na adhabu nyingine kali wapinzani wengi wa utawala huo lengo likiwa ni kukabiliana na uhuru wa kujieleza na kwa kisingizio cha ugaidi. 

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Kisaudia lenye makao yake barani Ulaya limetengaza kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Hukumu ya Kunyonga kwamba: Tokea kuanza mwaka huu wa 2022 hadi sasa Saudi Arabia imewanyonga watu 121.

Kesi 81 za watu kunyongwa kwa umati zimeripotiwa nchini humo; hali ambayo inatajwa kuwa mbaya zaidi ya watu kunyongwa kwa umati katika historia. Watu 41 kati ya hao walionyongwa walikuwa wapinzani wa madhehebu ya Kishia wa nchi hiyo na wenyeji wa maeneo ya al Ahsa na Qatif mashariki mwa Saudi Arabia. Tukio kama hilo la kunyongwa idadi hiyo kubwa ya Waislamu wa Kishia huko Saudia katika kipindi cha siku moja lilikuwa halijawahi kushuhudiwa tena nchini humo.