Hakuna nchi inayopasa kutuhofia iwapo haiwasaidii wavamizi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140932-hakuna_nchi_inayopasa_kutuhofia_iwapo_haiwasaidii_wavamizi
Iran imesema kuwa nchi hazipaswi kuwa na wasiwasi wowote kuhusu Jamhuri ya Kiislamu, isipokuwa pale zinapozipatia pande zinazotekeleza vitendo vya uhalifu na uvamizi vituo, miundombinu au zana ili kutekeleza mashambulizi dhidi yake.
(last modified 2026-08-24T13:51:14+00:00 )
Aug 24, 2026 13:49 UTC
  • Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei
    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei

Iran imesema kuwa nchi hazipaswi kuwa na wasiwasi wowote kuhusu Jamhuri ya Kiislamu, isipokuwa pale zinapozipatia pande zinazotekeleza vitendo vya uhalifu na uvamizi vituo, miundombinu au zana ili kutekeleza mashambulizi dhidi yake.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei amebainisha haya katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari mijini Tehran leo Jumatatu. Baghaei ameeleza hayo wakati akijibu maswali kuhusu taarifa katika vyombo vya habari vya Magharibi kwamba kambi za Marekani barani Ulaya zingeweza kulengwa iwapo nchi za Ulaya zingeshiriki tena katika vitendo vya uchokozi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

"Pia tumepata taarifa kwamba ndege kadhaa za mafuta aina ya KC-135 zimeondoka Bulgaria," amesema Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran. Ameongeza kuwa Iran imeweka wazi msimamo wake kuhusu Bulgaria na kwamba tangu awali wananchi na wanasiasa wa Bulgaria pia wameitaja hatua ya nchi hiyo ya Ulaya ya kuruhusu vituo vyake kutumiwa na Marekani dhidi ya Iran kuwa ni kinyume cha sheria za kimataifa.

"Hatuna tatizo na wananchi wa Bulgaria hata hivyo kushiriki kivyovyote katika hujuma zinazoilenga Jamhuri ya Kiislamu kunahesabiwa kuwa ni kitendo cha kichokozi," amesema Baghaei.

“Tunatumai kuwa nchi nyingine ambazo, kwa namna moja au nyingine, zimetoa vituo na miundombinu yake kwa Marekani na utawala wa Kizayuni ili kutekeleza uchokozi dhidi ya nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa nazo pia zitachukua hatua zinazostahili,”amesisitiza Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje.