Wapinzani Sudan wapinga mazungumzo ya kitaifa ya Burhan
-
Wapinzani wa Sudan
Mkutano mkubwa wa makundi ya kisiasa na asasi za kiraia za Sudan zinayopinga vita umemalizika huko Addis Ababa mji mkuu wa Ethiopia.
Makundi hayo yamekataa mazungumzo ya kitaifa yaliyopendekezwa na Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, yakisema kuwa hayatashiriki wala kutambua matokeo yake.
Makundi hayo yanasema kuwa mpango huo hauwezi kurejesha amani wakati mapigano yakiendelea, hasa ikizingatiwa kuwa wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kinachoongozwa na Jenerali Hemedti, hawakushirikishwa katika mazungumzo hayo.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok pia amesisitiza kuwa hakuna mchakato wa kuaminika wa amani unaoweza kufanikiwa bila ya mapigano kukomeshwa.
Washiriki wa mkutano wa Addis Ababa wamemtuhumu Jenerali Abdel Fattah al- Burhan kuwa anatumia mazungumzo hayo kuhalalisha mamlaka yake kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021.
Makundi ya kisiasa na asasi za kiraia za Sudan pia zimetahadharisha kuwa mpango huo unaweza kuzidisha mgawanyiko nchini Sudan.
Mkutano wa Addis umewakutanisha wanachama wa Chama cha Kongresi ya Taifa, Chama cha Umma, Muungano wa Amani wa Summud, na asasi za kiraia za Sudan.
Waziri Mkuu wa Sudan, Kamil Idris wiki iliyopita alitangaza kuwa mazungumzo ya ndani kati ya makundi mbalimbali ya Wasudani yataanza hivi karibuni, kwa lengo la kufikia maridhiano ya kina nchini humo na hatimaye kufanyika uchaguzi huru na wa haki.