Mabomu ya kutegwa ardhini, mabomu ya vishada na wahanga wa Yemen
Wananchi wa Yemen wanaokabiliwa na mashambulizi ya Saudi Arabia, sasa wamekuwa wahanga wa mabomu ya kutegwa ardhini silaha zilizoachwa nyuma na wavamizi hao.
Saudi Arabia ilianzisha vita dhidi ya Yemen mnamo Machi 26, 2015. Katika vita hivyo vya miaka 8, mabomu na silaha nzito zimekuwa zikitumiwa kushambulia Wayemeni katika maeneo tofauti ya nchi hii. Silaha na mabomu yaliyosalia katika ardhi ya Yemen sasa yamekuwa tatizo kwa raia wa kawaida, hasa wanawake na watoto, ambao ndio wahanga wakuu wa mabomu hayo.
Kituo cha kutegua mabomu ya chini ya ardhi cha Yemen kimetangaza kwamba mabaki ya mabomu ya muungano wa vita wa Saudia katika mikoa ya al Hudaydah, Sana'a, Al-Jawf na Sa'ada yanaendelea kuua raia wasio na hatia na kwamba watu 14 wauawa na wengine 16 wamejeruhiwa katika maeneo hayo mwezi uliopita wa Januari pekee. Ripoti ya kituo hicho imesema, nusu ya wahanga hao ni watoto wadogo, na mwezi huu wa Februari, ndani ya siku tatu tu, zaidi ya raia 10 wamejeruhiwa kutokana na milipuko wa mabomu ya kutegwa ardhini ya Saudi Arabia na washirika wake.
Hapo awali, Ofisi ya Mpango wa Maendeleo ya Umoja wa Mataifa ilitangaza kuwa tangu mwaka 2018, raia 1,800 wameuawa au kujeruhiwa na mabomu ya kutegwa ardhini na silaha ambazo hazijaripuka katika baadhi ya mikoa ya Yemen. Ripoti hiyo ya UN imeashiria kuwa wanawake na watoto wasiopungua 689 wa Yemen wameuawa kwa milipuko ya mabomu ya kutegwa ardhini na kuongeza kuwa: Mwaka 2021 timu za wahandisi za Umoja wa Mataifa zilifanikiwa kutegua mabomu 73,930 na mada nyingine za milipuko ambazo zilikuwa bado hazijaripuka. Wakati huo huo, kituo kinachosimamia uteguaji wa mabomu yaliyotegwa chini ya ardhi nchini Yemen hivi karibuni kiliripoti kuwa watu 734 waliuawa au kujeruhiwa mwaka jana (2022) kutokana na milipuko ya mabomu ya kutegwa ardhini na mabomu ya vishada nchini humo.
Idadi hii ya wahanga wa milipuko ya mabomu ya kutegwa ardhini na yale ya vishada inaonyesha jinsi muungano wa vita wa Saudi Arabia ulivyotumia kiwango kikubwa cha mabomu ya aina hiyo. Brigedia Jenerali Ali Safra, mkuu wa kituo cha uteguaji mabomu ya chini ya ardhi nchini Yemen, hivi karibuni alisema: "Tunakabiliwa na maafa. Mabomu ya vishada ya aina tofauti na yanayotengenezwa na nchi mbalimbali yametumika dhidi ya Yemen."
Licha ya maafa hayo, Saudia na washirika wake wa Kiarabu na Kimagharibi hawaruhusu kuingizwa nchini Yemen vifaa vya kugundua mabomu na zana nyinginezo za kivita zilizotegwa ardhini; jambo ambalo ni sababu ya kuongezeka idadi ya wahanga wa mabomu hayo nchini Yemen.
Suala jingine ni kwamba, kamati ya Umoja wa Mataifa ya ufuatiliaji wa Makubaliano ya al Hudaydah yenye jukumu la kudhamini utoaji wa vifaa, pia inapuuza hatua ya Saudia na washirika wake ya kukwamisha kazi hiyo na haichukui hatua za dhati kuwashawishi Wasaudia ili waruhusu vifaa vya kugundua mabomu yaliyotegwa ardhini kuingizwa nchini Yemen.
Kwa kutilia maanani hali hiyo, inabainika kuwa, hata kama usitishaji vita kati ya Wayemeni na Wasaudi utafikiwa, hatuwezi kusema kwamba maafa ya binadamu ya vita vya nchi hii yamekoma, kwa sababu mabomu ya kutegwa ardhini na yale ya vishada yaliyoachwa katika maeneo mbalimbali ya Yemen kutokana na mashambulizi ya miaka 8 ya Saudi Arabia na washirika wake yanaendelea kusababisha vifo vya raia wasio na hatia.