Ndege za kivita za Saudia zadondosha mabomu msikitini kaskazini mwa Yemen
Ndege za kivita za Saudia zadondosha mabomu katika msikiti mmoja uluoko mkoa wa Al Jauf kaskazini mwa Yemen.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Yemen Saba, ndege za kivita za Saudia katika kuendeleza ukiukwaji wa mapatano ya kivita zimeshambulia Masjid Munif katika eneo la al Matun mkoani Jauf wakati waumini walipokuwa wakiondoka sikitini hapo baada ya kumaliza sala. Duru zinaarifu kuwa watu kadhaa wamejeruhiwa na jengo la msikiti kuharibiwa vibaya.
Hii si mara ya kwanza kwa ndege za kivita za Saudia kudondosha mabomu katika misikiti ya Yemen tokea ianzishe vita dhidi ya nchi hiyo mwezi Machi mwaka 2015.
Aidha ndege za Saudia hudondosha mabomu katika mahospitali, shule, viwanda na mabwawa ya maji kama njia ya kuwashinikiza watu wa Yemen wasalimu amri. Hata hivyo Saudia haijaweza kufanikiwa kufikia malengo yake hayo, bali watu wa Yemen wanaendeleza mapambano ya kukabiliana na wavamizi wa kigeni wanaoongozwa na Saudia.
Saudia na baadhi ya nchi za Kiarabu ziliivamia Yemen mwezi Machi 2015 kwa baraka kamili za Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa madai ya kumrejesha madarakani kibaraka wao, Abdu Rabuh Mansour Hadi, lakini wameshindwa.
Maelfu ya wananchi wa Yemen wakiwemo mamia ya wanawake na watoto wadogo wameshauawa na wengine wengi kujeruhiwa na asilimia 80 ya miundombinu ya Yemen kuharibiwa kikamilifu hadi hivi sasa.