Shahidi Khader Adnan; nembo ya muqawama katika mapambano dhidi ya Israel
Utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya jinai kubwa ya kumuua Sheikh Khader Adnan akiwa gerezani.
Sheikh Khader Adnan, mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa harakati ya Jihadul Islami ya Palestina amekufa shahidi baada ya kugoma kula kwa siku 86 akiwa katika jela ya kutisha ya utawala wa Israel.
Davoud Shihab, Msemaji wa Harakati ya Jihadul Islami ya Paleitna alisema jana Jumanne alipohojiwa na shirika la habari la Iran Press kwamba: Mapambano yanaendelea licha ya kuuliwa shahidi Sheikh Khader Adnan na kwamba, jinai hiyo ya Wazayuni maghasibu itaimarisha azma ya Wapalestina ya kuendeleza njia ya Sheikh Adnan.
Wizara inayoshughulikia masuala ya Wapalestina wanaoshikiliwa mateka na walioachiwa huru nayo imetangaza kuwa, Sheikh Khader Adnan, mfungwa Mpalestina amekata roho na kufa shahidi ndani ya gereza la utawala haramu wa Kizayuni.
Adnan, mmoja wa viongozi wa harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina, alikamatwa na utawala wa Kizayuni Februari 5 na kuamua kususia kula kwa muda wa siku 86 mfululizo akipinga kuwekwa kizuizini kiidara.
Msemaji wa Jihadul- Islami ya Palestina ameongeza kuwa, Sheikh Khader Adnan alikuwa shakhsia mtajika na mpigania ukombozi mkubwa. Aidha alifanya juhudi za kihistoria na kubwa katika kipindi chote cha mapambano yake dhidi ya utawala haramu wa Israel.
Khader Adnan miaka kadhaa iliyopita aligoma kula mara sita lengo likiwa ni kufikisha sauti ya wafungwa wote wa Kipalestina kwa walimwengu na kila wakati aliweza kuachiwa huru baada ya kugoma kula.