Mawaziri wa nchi za Kiarabu wakubaliana Syria kurejeshwa katika Arab League
May 07, 2023 06:55 UTC
Chaneli ya televisheni ya Al-Arabiyya imetangaza kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu wamekubaliana katika mkutano wao uliofanyika leo mjini Cairo kurejeshwa Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League).
Mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wamefanya kikao cha dharura katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje mjini Cairo kujadili kadhia ya Syria, zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kabla ya mkutano wa wakuu wa nchi za Kiarabu utakaofanyika mjini Riyadh, Saudi Arabia mnamo Mei 19.
Televisheni ya Al-Arabiya inayomilikiwa na Saudi Arabia imeripoti kuwa katika mkutano wao wa mashauriano uliofanyika kwa faragha leo, mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wamekubaliana juu ya kurejea Syria kwa masharti katika jumuiya hiyo baada ya kutokuwepo kwa takriban miaka 12.
Al-Arabiya imetangaza kuwa katika rasimu ya uamuzi huo, ambayo itachapishwa rasmi hapo baadaye imeelezwa kuwa: "kuanzia leo Mei 7, ushiriki wa wajumbe wa Syria katika mikutano ya jumuiya hii utaanza tena".
Awali kabla ya hapo, Jamal Rushdi, msemaji wa Arab League alisema kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya hiyo wataamua juu ya kufuta uamuzi wa kusimamishwa uwanachama wa Syria.
Rushdi alifafanua kuwa, katika mkutano huo, matokeo ya mikutano ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu iliyofanyika Saudi Arabia na Jordan kwa ajili ya kuirejesha Syria katika jumuiyo hiyo na uamuzi wa kuialika Damascus katika kikao kijacho cha wakuu wa Arab League kitakachofanyika mjini Riyadh itajadiliwa.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Jordan, Saudi Arabia, Iraq, Misri na Syria walifanya mkutano wa mashauriano wiki iliyopita kujadili njia za kuwarejesha wakimbizi wa Syria kutoka nchi jirani na kupanua udhibiti wa serikali ya Damascus katika maeneo yote ya nchi hiyo pamoja na kutatua suala la biashara haramu ya madawa ya kulevya.
Mkutano huo ulifanyika kufuatia mkutano mwingine wa mawaziri wa mambo ya nje wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi uliofanyika katikati ya mwezi uliopita wa Aprili nchini Saudia kujadili kurejea Syria katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, ambapo mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Iraq na Jordan walishiriki pia.
Mnamo Novemba 2011, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilisimamisha uwanachama wa Syria na kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kisiasa na kiuchumi.../