Mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Gaza yalaaniwa kimataifa
Lawama za kimataifa zimeongezeka baada ya utawala haramu wa Israel kufanya mashambulizi mapya ya anga dhidi ya Ukanda wa Gaza na kusababisha Wapalestina 13 kufa shahidi na wengine 20 kujeruhiwa.
Katika taarifa yake siku ya Jumanne, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imelaani mashambulizi ya hivi punde zaidi ya Israel dhidi ya eneo hilo la Palestina lililozingirwa na kusema jinai hizo zitaimarisha tu azma ya wananchi wa Palestina ya kuendeleza mapambano yao dhidi ya utawala huo ghasibu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jordan pia imelaani hujuma ya Israel dhidi ya Gaza katika taarifa, ikisema kuwa Amman itaendelea na juhudi zake za kukomesha ghasia mara moja na kurejesha utulivu.
Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki imeyataja mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza kuwa yasiyokubalika, ikibainisha kuwa Ankara inatarajia kuwa mvutano huo utakomeshwa mara moja kabla ya kusababisha migogoro mipya katika eneo.
Zaidi ya hayo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imelaani vikali mashambulizi ya hivi punde zaidi ya Israel dhidi ya Gaza, ikisema kuwa ni kinyume cha sheria za kimataifa.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) pia imelaani "uhalifu wa kinyama" unaofanywa na Israel huko Gaza, na kuitaka jumuiya ya kimataifa itekeleze wajibu wake wa kuwaunga mkono Wapalestina na kuuwajibisha utawala wa Israel.
Naye Tor Wennesland, mratibu maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Mashariki ya Kati, amelaani mashambulizi hayo ya anga ya Israel ambayo yamesababisha vifo vya raia wa Palestina.
Amesema, "Mashambulizi ya anga ya Israel ndani ya Gaza yamesababisha mauaji ya Wapalestina 13, wakiwemo wanachama watatu wa Jihad Islami, daktari, wanawake watano na watoto wanne, na zaidi ya 20 kujeruhiwa. Nalaani vifo vya raia katika mashambulizi ya anga ya Israel. Hili halikubaliki,” ameongeza.
Mapema siku ya Jumanne, ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel zilifanya mashambulizi kadhaa kwenye Ukanda wa Gaza, na kuwauwa makamanda watatu mashuhuri wa harakati ya mapambano ya Jihad Islami ya Palestina.
Takriban Wapalestina 13 wameuawa shahidi katika mashambulizi hayo na wengine 20 kujeruhiwa, huku maeneo kadhaa katika mji wa Gaza, Rafah na Khan Yunis yakilengwa kwa mabomu ya Israel.