Unicef yaonya kuhusu tishio la njaa kwa watoto wa Yemen
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) limetangaza kuwa mamilioni ya watoto huko Yemen wamebakiza hatua moja tu kukumbwa na njaa.
Kituo cha Haki za Binadamu cha Ain kiliwahi kuripoti kuwa, raia wa Yemen 18,140 wameuawa na wengine elfu 30,254 wamejeruhiwa katika kipindi cha miaka minane ya kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu nchi yao na Muungano vamizi wa Saudia na Marekani.
Utafiti uliofanywa na kituo hicho unaonyesha kuwa, mtoto mmoja huaga dunia katika kila dakika 6 nchini Yemen kwa sababu ya njaa huku Wayemeni wengine miloni 17 wakikabiliwa na ukosefu wa chakula.
Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, Shirika la Unicef limetaka kuchukuliwe hatua kimataifa haraka iwezekanavyo kudhamini fedha za kutosha na kutoa misaada ili kunusuru maisha ya Wayemeni.
Unicef aidha imesisitiza katika ripoti yake ya huko nyuma kwamba watoto milioni 11 wanahitaji misaada ya kibinadamu huko Yemen na kwamba kati ya iiadi hiyo, watoto zaidi ya laki tano na arubaini elfu walio na umri wa chini ya miaka mitano wanasumbuliwa na utapiamlo mkali; hali inayotishia maisha yao.
Saudi Arabia ikiungwa mkono na kupewa himaya na Marekani, Imarati na nchi nyingine kadhaa, ziliivamia Yemen mwezi Machi 2015 na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, anga na nchi kavu.