Azimio la WHO: Tel Aviv idhamini afya ya Wapalestina
Shirika la Afya Duniani (WHO) jana lilipasisha azimio kuhusu hali ya kiafya huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na wajibu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao umetakiwa kudhamini afya ya raia wa Palestina.
Azimio hilo lilipasishwa kwa kura 76 za ndio, 13 za hapana na nchi 35 hazikupiga kura. Azimio hilo lilipasishwa baada ya kuchunguzwa rasimu ya muswada kuhusu hali ya kiafya ya raia katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ikiwemo Quds Tukufu na katika miinuko ya Golan ya Syria iliyovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Israel.
Azimio hilo linalenga kufuatilia mahitaji ya kiafya ya raia katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Azimio hilo linaeleza kuwa: Kukosekana usimamizi wa afya katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu ni changamoto kubwa kwa utoaji wa huduma bora za afya kwa raia wa Palestina.
Azimio hilo linasema: Israel ukiwa ni utawala ghasibu, ina jukumu la kulinda afya na kutambua haki ya afya ya Wapalestina wote wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Baitul Muqaddas ya Mashariki na Ukanda wa Gaza.
Azimio la Shirika la Afya Duniani kuhusu Palestina aidha limebainisha kuwa, jukumu la Israel ni pamoja na kuhakikisha kuwa kunakuwepo usawa na kuacha ubaguzi katika utoaji huduma za afya na kuwadhaminia raia wa Paestina haki yao ya kiafya.