Marekani inapanga kujenga kituo cha pili cha kijeshi magharibi ya Iraq
May 26, 2023 03:12 UTC
Duru moja ya masuala ya usalama ya Iraq imefichua kuwa wanajeshi magaidi wa Marekani wanapanga kujenga kambi mpya ya kijeshi katika mkoa wa al-Anbar ulioko magharibi mwa Iraq.
Marekani tayari imejifaragua kijeshi magharibi mwa Iraq, hasa katika kambi ya Ain al-Asad. Kambi hiyo ni ya pili kwa ukubwa ya Marekani nchini Iraq baada ya kambi ya jeshi la anga ya Balad, iliyoko katika eneo la Al-Baghdadi, iliyovamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu na Marekani mwaka 2003 na hadi leo ikiendelea kuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo.
Tovuti ya habari za uchambuzi ya The Cradle imenukuu duru moja ya masuala ya usalama ya Iraq ikisema kuwa Jeshi la Marekani limechagua eneo la Al Jazeera kujenga kambi yake ya kijeshi, kwa sababu eneo hilo lina akiba kubwa ya mafuta na gesi.
The Cradle imeendelea kueleza katika ripoti yake kwamba, duru za kuaminika za Iraq hapo awali ziliripoti kuwa majeshi ya Marekani hayana nia ya kuondoka nchini humo, bali yanatafuta njia ya kuipanua zaidi kadiri inavyowezekana kambi ya Ain al-Asad iliyoko katika mkoa wa al-Anbar.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Wamarekani wanafanya juu chini kupanua uwepo wao wa kijeshi nchini Iraq na wametumia madai ya kupambana na mabaki ya magaidi waliotawanyika wa DAESH (ISIS) kama kisingizio cha kuwepo kwao kivamizi ndani ya ardhi ya nchi hiyo.
Wananchi na makundi mengi ya Iraq yanataka vikosi vya wanajeshi magaidi wa Marekani viondoke nchini Iraq, na bunge la nchi hiyo pia limeidhinisha mpango wa kuondolewa vikosi hivyo katika ardhi ya nchi hiyo.../