Sana'a yionya Riyadh kuhusu "jibu kali litakaloifanya ijute"
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i98182-sana'a_yionya_riyadh_kuhusu_jibu_kali_litakaloifanya_ijute
Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ameutahadharisha muungano wa vita unaoongozwa na Saudi Arabia kwamba iwapo utaendelea kuchelewesha na kupoteza muda katika mazungumzo ya amani, utakabiliwa na jibu la kushtukiza na litakaloufanya ujute.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 29, 2023 22:08 UTC
  • Sana'a yionya Riyadh kuhusu

Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ameutahadharisha muungano wa vita unaoongozwa na Saudi Arabia kwamba iwapo utaendelea kuchelewesha na kupoteza muda katika mazungumzo ya amani, utakabiliwa na jibu la kushtukiza na litakaloufanya ujute.

Yasser Al-Houri, Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesisitiza kuwa: Iwapo Saudi Arabia iitaendelea kuchelewesha mazungumzo ya amani, Sana'a itazingatia njia na machaguo mbadala, kwa kutilia maanani bidhaa za kijeshi zinazotengenezwa nchini. 

Al-Houri ameongeza kuwa: Saudi Arabia inajaribu kuvuta muda katika kutekeleza majukumu yake kuhusiana na faili la masuala ya kibinadamu nchini Yemen, na kama hakutakuwa na dhamira ya wazi, Saudi Arabia na eneo zima la Asia mashariki hazitapata usalama na utulivu.

Katibu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen ameeleza kuwa: Suala la kukabiliana na athari za uvamizi uliofanywa na Saudia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen ni kubwa zaidi ya kulipa fidia na ujenzi mpya, kwa sababu linajumuisha nyanja zote za kimaadili, kisaikolojia, kiafya na kadhalika.

Duru ya kwanza ya mazungumzo ya amani baina ya Yemen na Saudi Arabia ilifanyika Aprili 10 kwa ziara ya balozi wa Saudi Arabia nchini Yemen, Muhammad Al-Jaber, huko Sana'a, na pande hizo zilikubaliana kuwaachilia huru wafungwa 900 kutoka pande zote mbili ili kuonyesha nia njema.

Tangu wakati huo hakuna hatua nyingine ya maana iliyochukuliwa kwa ajili ya kukomesha maafa yanayowapata watu wa Yemen kutokana na hujuma na mashambulizi ya miaka kadhaa ya Saudi Arabia na washirika wake.