Hizbullah yasema iko tayari na inafuatilia yanayojiri Kafr Shuba
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa inafuatilia yanayojiri katika eneo la Kafr Shuba na uchokozi uliofanywa na askari wa utawala haramu wa Israel katika ardhi ya Lebanon.
Itakumbukwa kuwa, askari wa utawala ghasibu wa Israel mapema jana Ijumaa walirusha mabomu ya kutoa machozi karibu na eneo liliko jeshi la Lebanon Kusini mwa nchi hiyo; na kufuatia kitendo hicho cha Wazayuni, wananchi wa eneo la Kafr Shuba walipambana vikali na askari hao wa Israel.
Mtandao wa televisheni ya Al-Manar umemnukuu Ali Fayaz, mwanachama wa kikundi cha Al-Wafaa cha harakati ya Hizbullah, akisisitiza kwamba harakati hiyo inafuatilia matukio yanayojiri kwenye miinuko ya Kafr Shuba.
Fayaz ameongeza kuwa Hizbullah iko tayari kwa ajili ya kukabiliana na uwezekano wa kujitokeza mvutano katika eneo hilo na kamwe haitamruhusu adui wa Israel kuendelea na uchokozi wake.
Aamesisitiza kuwa, adui Mzayuni anajua kwamba kung'ang'ania kuvuka mistari myekundu kutakuwa na gharama kubwa kwake.
Mjumbe huyo wa Hizbullah pia amepongeza msimamo wa jeshi la Lebanon kuhusu yanayojiri eneo la Kusini mwa nchi hiyo na kusema kwamba vuguvugu la wananchi la kukabiliana na askari wa Israel limetegemea msimamo thabiti wa kutetea mamlaka ya nchi, na kwamba Hizbullah haitazembea kutetea nchi na wananchi wa Lebanon.
Ripoti zinasema baada ya uchokozi huo wa Israel, jeshi la Lebanon lilijiweka katika hali ya vita kwa ajili ya kukabiliana na wanajeshi wa Israel kwenye eneo la mpakani la Kafr Shuba.