UN yatahadharisha kuhusu hatari ya mamia ya Wapalestina kufukuzwa Quds (Jerusalem)
Afisa wa Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu hatari ya kufukuzwa na kukosa makazi mamia ya Wapalestina wa Quds Tukufu (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu.
Lynn Hastings, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika Maeneo ya Palestina Yanayokaliwa kwa Mabavu, ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel utawatimua watu wa familia ya Kipalestina ambao wanaishi katika eneo la kale la Quds (Jerusalem) tangu mwaka 1954.
Utawala wa Kizayuni wa Israel uliipa familia hiyo ya Kipalestina hadi Jumapili hii kuhama nyumba yao iliyoko Quds Mashariki na kuikabidhi kwa walowezi wa Kiyahudi.
Hastings amesema kuwa mamia ya Wapalestina wengine huko Quds Mashariki sasa wako katika hatari ya kufukuzwa katika makazi yao, na hii ni hatua mbaya ambayo inakiuka sheria za kimataifa na lazima ikomeshwe mara moja.
Ofisi ya Umoja wa Ulaya katika Maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu pia ilionya Alhamisi iliyopita kwamba familia 150 za Wapalestina huko Quds (Jerusalem Mashariki) ziko hatarini kufukuzwa katika makazi yao.
Umoja wa Ulaya pia metangaza upinzani wake dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Utawala wa Kizayuni wa Israel unajaribu kubadilisha muundo wa kijiografia wa maeneo ya Palestina na kuyapa maeneo hayo sura ya Kiyahudi kwa kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kwenye maeneo hayo, ili kuimarisha utawala wake kwenye ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina.