Wazayuni waendelea kubomoa nyumba za Wapalestina
Utawala ghasibu wa Israel umeendeleza jinai zake dhidi ya raia wa Kipalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kwa kubomoa nyumba za familia 5 za Kipalestina.
Duru za ndani ya Palestina zimetanagza kuwa, Wazayuni jana Jumatatu walivamia kijiji cha Arareh al Naqab katika ardhi ya Palestina iliyovamiwa mwaka 1948 na kubomoa kikamilifu nyumba za familia tano wa Wapalestina. Utawala wa Israel unabomoa nyumba za raia wa Kipalestina katika eneo hilo lengo likiwa ni kuwaweka chini ya mashinikizo na kuwafukuza raia hao katika eneo hilo.
Utawala haramu wa Israel umekuwa ukibomoa nyumba za raia wa Palestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi mahali pake lengo kuu likiwa ni kubadili muundo wa kijiografia wa maeneo ya Palestina na kuyapa maeneo hayo sura ya Kiyahudi.
Hii ni licha ya kwamba, azimio nambari 2334 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinataja shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi iliyoghusubiwa ya Palestina kuwa ni kinyume cha sheria; Hata hivyo utawala haramu wa Israel unaendeleza ubabe wake kwa kuharibu nyumba za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni mahali pale.
Siku kadhaa zilizopita Lynn Hastings, Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa katika Maeneo ya Palestina Yanayokaliwa kwa Mabavu, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel utawatimua watu wa familia ya Kipalestina ambao wanaishi katika eneo la kale la Quds (Jerusalem) tangu mwaka 1954.
Hastings amesema kuwa mamia ya Wapalestina wengine huko Quds Mashariki sasa wako katika hatari ya kufukuzwa katika makazi yao, na hii ni hatua mbaya ambayo inakiuka sheria za kimataifa na lazima ikomeshwe mara moja.