Hizbullah: Makubaliano ya Iran na Saudia yamesambaratisha njama za Marekani
Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, makubaliano ya Iran na Saudi Arabia ya kuhuisha uhuusiano wao wa kidiplomasia yamesambaratisha njama na mipango michafu ya Marekani.
Samahat Sheikh Naim Qassim ameeleza kuwa, Marekani imetangaza waziwazi kwamba, haijafurahishwa na makubaliano haya kama ambavyo hairidhishwi na matukio yanayoshuhudiwa sasa ambayo ni matokkeo ya makubaliano hayo.
Sheikh Naim Qassim amebainisha kwamba, hasira hizi za Marekani zinaonyesha kuwa, mipango yake kwa ajili ya eneo la Asia Magharibi imefeli na kugonga ukuta.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ameongeza kusema kuwa, mataifa ya eneo na harakati za kupigania ukombozi zinapaswa kutumia fursa hii vyema na hivyo hilo kuwa kwa maslahi ya eneo hili.
Tarehe 10 Machi mwaka huu na baada ya siku kadhaa za mazungumzo mazito yaliyosimamiwa na China, hatimaye Iran na Saudi Arabia zilikubali kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia na kufungua tena balozi zao.
Katika taarifa yao ya pamoja baada ya kusaini makubaliano hayo, Tehran na Riyadh zilisisitizia haja ya kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa ya kila mmoja na kujiepusha na kuingilia masuala ya ndani ya kila mmoja wao.
Makubaliano ya kuhuisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Saudia yamefuatiwa hatua kadha chanya kama na nchi hizo kufungua tena balozi zao, Syria kurejea katika Jumuiya ya nchi za Kiarabu, kuafikiana Saudia na Syria kufungua tena balozi zao na mataifa kadhaa ya Kiarabu kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia na mataifa ya Iran na Syria.