Hizbullah yataka jamii ya Kimataifa iuchukulie hatua utawala haramu wa Israel
Harakati ya Mapambano ya Kiiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imeitaka jamiii ya kimataifa kuuchukulia hatua utawala haramu wa Israel kutokana na vitendo vyake mbalimbali vya jinai na kuvunjiia heshima matukufu ya Kiislamu.
Hizbullah imetoa wito huo baada ya Wazayuni kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu na misikiti na kuzitaka nchi za Kiarabu, Kiislamu na asasi za kimataifa kuuchukulia hatua utawala huo wa kibaguzi.
Taarifa ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeeleza kwamba, hatua hiyo ya Wazayuni ni ugaidi wa hali ya juu kabisa, ubaguzi wa wazi na uvunjiaji heshima matukufu ya kidini.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kwamba, vitendo vya kuvunjia heshima matukufu na thamani za kidini vinavyofanywa na Wazayuni vinakinzana bayana na ubinadamu, maadili, utu na thamani za kiutu.
Ijumaa ya jana (Juni 23) walowezi wa Kizayuni walivamia Msikiti wa al-Ribat katika kitongoji cha Urif kusini mwa mji wa Nablus, na kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu.
Video ya kamera ya CCTV imeonyesha Wazayuni hao waliokuwa wamefunika nyuso zao wakichana na kuchoma moto nakala za Qurani Tukufu ndani ya msikiti huo. Walowezi hao wa Kizayuni hawakuishia hapo, bali walienda mbali zaidi na kuingiza mbwa ndani ya msikiti huo.
Katika taarifa yake, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani kitendo cha walowezi wa Kizayuni huko Nablus cha kuvamia misikiti na kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu na kusisitiza kuwa: Hii ni jinai ya kinyama inayochochea vita vya kidini vya taasisi za Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina.