Wamarekani: Biden na Trump hawafai kuingoza tena Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i100146-wamarekani_biden_na_trump_hawafai_kuingoza_tena_marekani
Aghalabu ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa, Rais wa sasa wa nchi hiyo, Joe Biden na mtangulizi wake, Donald Trump hawastahili kuiongoza nchi hiyo kwa muhula mwingine.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jul 21, 2023 04:11 UTC
  • Wamarekani: Biden na Trump hawafai kuingoza tena Marekani

Aghalabu ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa, Rais wa sasa wa nchi hiyo, Joe Biden na mtangulizi wake, Donald Trump hawastahili kuiongoza nchi hiyo kwa muhula mwingine.

Utafiti uliofanywa na mashirika ya Yahoo News/YouGov kwa kushirikisha Wamarekani 1,638 baina ya Julai 13 na 17 umefichua kuwa, asilimia 55 ya wananchi wa Marekani hawataki Biden agombee muhula wa pili wakisisitiza kuwa hana uwezo, umahiri na ustahiki wa kuliongoza tena taifa hilo.

Aidha asilimia 53 ya walioshirikishwa kwenye utafiti huo wamesema mtangulizi wa Biden, Donald Trump ambaye aliongoza kwa muhula mmoja, hafai kuliongoza tena taifa hilo kwani ni mwanasiasa fisadi, mtepetevu na hatari.

Asilimia 20 ya walioshiriki utafiti huo wa maoni wanasema Biden hafai kuwaongoza tena kutokana na utepetevu wake, asilimia 12 wanasema hafai kutokana na ukongwe wake, asilimia 10 wanasema ni mtu fisadi, asilimia 9 wanasema kiongozi huyo hafai kwa kuwa hivi sasa anapohudumu muhula wa kwanza hafanyi kazi ya kuridhisha, na asilimia 3 wanasema mwanaiasa huyo ni mtu hatari.  

Biden alivyokula mweleka hivi karibuni kutokana na ukongwe

Utafiti huo wa Yahoo News umefichua kuwa, asilimia 60 ya Wamarekani, nusu wakiwa ni wafuasi wa chama cha Democrats wanaitakidi kuwa, Marekani ipo katika mkondo mbaya na inaelekea kusiko.

Aidha asilimia 92.8 ya wafuasi wa chama cha Republican walioshirikishwa kwenye utafiti huo wa maoni wanaona kuwa, Biden ameshindwa kutekeleza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni ya kuwaunganisha Wamarekani.

Haya yanajiri siku chache baada ya utafiti mwingine uliotolewa na shirika la Trafalgar kuonesha kuwa, Biden amevunja rekodi ya kushuka umashuhuri wake baina ya Wamarekani.