Korea Kaskazini yakosoa msaada wa silaha za Marekani kwa Taiwan
(last modified Fri, 04 Aug 2023 07:51:33 GMT )
Aug 04, 2023 07:51 UTC
  • Korea Kaskazini yakosoa msaada wa silaha za Marekani kwa Taiwan

Korea Kaskazini imekosoa vikali hatua ya Marekani ya kuipa Taiwan msaada wa silaha wa mamilioni ya dola ikisisitiza kuwa, Washington inakitumia kisiwa hicho kinachojitawala kushadidisha taharuki na kuchochea moto wa vita katika eneo.

Shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA limemnukuu Maeng Yong Rim, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Masuala ya China katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini akisema leo Ijumaa kuwa, mpango huo wa Marekani si tu ni hatua hatari ya kisiasa na uchokozi wa kijeshi, lakini pia unakanyaga kanuni ya China Moja.

Hii ni baada ya Marekani kuzindua kifurishi cha msaada wa kijeshi kwa Taiwan wenye thamani ya dola milioni 345; huku Kongresi ya US ikiidhinisha kupewa eneo hilo silaha zenye thamani ya dola bilioni 1, kama sehemu ya bajeti yake ya mwaka huu 2023.

Mapema mwezi uliopita pia, China ilikosoa vikali mpango mpya wa serikali ya Marekani wa kuiuzia Taiwan silaha zenye thamani ya mamilioni ya dola, ikisisitiza kuwa mauzo hayo yanakiuka kanuni ya "China Moja".

China ilitangaza msimamo huo baada ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kusema kuwa imeidhinisha mkataba wa kuiuzia silaha Taiwan utaogharimu dola milioni 440.

Bendera za Taiwan na Marekani

Viongozi wa China wamekuwa wakiionya Washington kuhusu kuendelea kuiuzia Taiwan silaha wakisisitiza kuwa, baadhi ya maafisa nchini Marekani wanataka kuitumia Taiwan kuidhibiti China, lakini wanapaswa kujua kwamba vitendo hivi ni hatari sana, na ni sawa na kucheza na moto. 

Serikali ya Beijing imekuwa ikisisitiza kuwa, Taiwan ni sehemu ya ardhi kuu ya China na kwamba chaguo la kutumia nguvu za kijeshi ili kushika hatamu za udhibiti wa kisiwa hicho lipo mezani.