Maoni: Ukosefu wa usalama umeongezeka Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i10078-maoni_ukosefu_wa_usalama_umeongezeka_marekani
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni yameonesha kuwa, Wamarekani wengi wanaamini kuwa, nchi hiyo inakabiliwa na ukosefu wa amani mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 27, 2016 15:59 UTC
  • Maoni: Ukosefu wa usalama umeongezeka Marekani

Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni yameonesha kuwa, Wamarekani wengi wanaamini kuwa, nchi hiyo inakabiliwa na ukosefu wa amani mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na kampuni ya Rasmussen Reports ambayo matokeo yake yametolewa leo, unaonesha kuwa, asilimia 74 ya Wamarekani wanaamini kuwa, nchi hiyo inasumbuliwa na ukosefu wa amani kuliko ule wa kabla ya mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001.

Matokeo ya uchunguzi huo yanasema asilimia 26 tu ya Wamarekani ndio wanaoamini kuwa Marekani ina amani zaidi kuliko kipindi cha kabla ya mashambulizi ya Septemba 11.

Takwimu hizo kuhusu usalama wa Marekani zinaakisi kiwango cha chini sana cha imani ya Wamarekani kwa usalama wa nchi hiyo tangu mwaka 2006.

Mauaji ya kutumia silaha katika maeneo ya umma kama mashuleni, vilabuni, ofisini na kadhalika yamekithiri sana nchini Marekani katika miezi ya hivi karibuni. Tarehe 12 mwezi huu wa Juni watu wasiopungua 50 waliuawa na wengine 53 kujeruhiwa baada ya kumiminiwa risasi katika jimbo la Florida nchini Marekani.