Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Pakistan atiwa nguvuni
Waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Pakistan ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa chama cha Tehreek-e-Insaf Pakistan amekamatwa na kuwekwa kizuizini na vyombo vya usalama mjini Islamabad.
Shirika la habari la IRNA limevinukuu vyombo vya habari vya Pakistan na kuripoti kuwa, Shah Mehmood Qureshi, ambaye ni kiongozi nambari mbili wa chama cha waziri mkuu wa zamani Imran Khan, alikamatwa mjini Islamabad saa chache baada ya mkutano wake na waandishi wa habari jana Jumamosi. Hii ni mara ya pili kwa Qureshi kukamatwa na vyombo vya usalama katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Inasemekana kuwa kukamatwa kwa Qureshi kunahusiana na kufichuliwa kwa barua ya siri, ambayo Imran Khan anadai kuwa ni sehemu ya mashinikizo ya Marekani ya kutaka kuipindua serikali yake mnamo mwaka 2022.
Kwa mujibu wa ufichuaji huo, maafisa wawili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, walikutana na balozi wa Islamabad mjini Washington, ambapo katika mazungumzo hayo waliihimiza Pakistan imuondoe Imran Khan katika wadhifa wa uwaziri mkuu kwa sababu ya kutangaza kutoegemea upande wowote katika vita vya Ukraine.
Naibu Kiongozi huyo wa chama Tehreek-e-Insaf Pakistan alikamatwa miezi mitatu iliyopita pia kufuatia kutiwa nguvuni kiutatanishi Imran Khan kwa tuhuma za kuwachochea watu kufanya fujo, lakini baada ya mwezi mmoja na nusu aliachiliwa kwa dhamana.
Kiongozi wa chama cha Tehreek-e-Insaf Pakistan Imran Khan alikamatwa na kupelekwa gerezani Agosti 5 mwaka huu baada ya hakimu wa mahakama ya kupambana na ufisadi kumpata na hatia katika kesi ya ufisadi na kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela na kumpiga marufuku pia kushika wadhifa wowote wa serikali na wa kisiasa.../