Jun 29, 2016 07:26 UTC
  • Ban Ki-moon alaani mashambulizi ya kigaidi huko Istanbul Uturuki

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa kwenye uwanja wa ndege wa Istanbul Uturuki.

Ban Ki -moon Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa na kulaani mashambulizi ya kigaidi ya jana usiku katika uwanja wa ndege wa Istanbul na kutaka kuwepo ushirikiano mkubwa wa kimataifa katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Ban Ki-moon pia ametoa mkono wa pole kwa familia za wahanga na kwa serikali ya Uturuki kufuatia mashambulizi hayo ya kigaidi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anataraji kuwa watu waliohusika na jinai hiyo watatambuliwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Ban Ki-moon amesema kuna udharura wa kuzidishwa jitihada za kieneo na kimataifa katika mapambano dhidi ya ugaidi na vitendo vya uchupaji mipaka na kueleza kuwa, yuko pamoja na Uturuki katika vita dhidi ya tishio hilo. Watu waliokuwa na mada za miripuko jana usiku waliingia katika uwanja wa ndege wa Ataturk mjini Istanbul na kuripua mada hizo katika maeneo matatu ya uwanja huo wa ndege. Duru za habari zimearifu idadi ya watu waliopoteza maisha katika mashambulizi hayo ya kigaidi kuwa ni 36 na zaidi ya 140 wamejeruhiwa.

Tags