China: Haiwezekani Taiwan kupewa uanachama wa UN
(last modified Sat, 16 Sep 2023 04:43:28 GMT )
Sep 16, 2023 04:43 UTC
  • China: Haiwezekani Taiwan kupewa uanachama wa UN

Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa amesema jitihada za maajinabi zinazoendelea za eti kutafuta uhuru wa Taiwan zitafeli.

Vyombo vya habari vya China vimeripoti hiyo habari hiyo Ijumaa, ambapo vimemnukuu Zhang Jun, Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa ambaye amekosoa hatua ya Taipei ya kumuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia waitifaki wake, kutaka Taiwan ipewa uanachama katika UN.

Jun amesema, "Kile kinachoitwa ushiriki wa Taiwan katika Umoja wa Mataifa ni simulizi bandia, na kwamba kuna China moja duniani, na Taiwan ni sehemu isiyotengenishika na ardhi ya China."

Mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, njama za kutaka kuitumia Taiwan kudhibiti China zitafeli na kugonga mwamba.

Hivi karibuni pia, Mao Ning, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alikosoa mashinikizo ya kutaka kupewa uhuru Taiwan na kupewa uanachama katika Umoja wa Mataifa akisisitiza kuwa, "Daima kuna kiti kimoja tu cha kuiwakilisha China UN." 

Serikali ya China ambayo inasisitiza kuwa Taiwan ni sehemu ya ardhi yake imekuwa ikisisitiza kuwa, itachukua hatua kali na madhubuti ikiwemo ya kijeshi, kutetea mamlaka yake ya kujitawala na umoja wa ardhi yake yote.