Makumi ya wanawake wamshtaki daktari Mmarekani kwa kuwadhalilisha kingono
Wanawake 82 nchini Marekani wamemfungulia mashtaka daktari aliyekuwa akifanya katika hospitali moja katika mji wa Boston nchini humo kwa tuhuma za kuwadhalilisha kingono.
Daktari huyo (Rheumatologist) aliyefahamika kwa jina la Derrick Todd, mfanyakazi wa zamani katika Hospitali ya Brigham mjini Boston ambaye alijiuzulu msimu huu wa joto baada ya kuanza uchunguzi mkubwa kuhusu madai ya kuwadhalilisha kijinsia wanawake anakabiliwa na makumi ya mashtaka mapya.
Drew Meyer, Wakili aliyewasilisha kesi hiyo katika Mahakama Kuu ya Suffolk, anasema wanawake 82 wamejiunga na kesi hiyo hadi sasa. Hii ni kesi ya tatu dhidi ya Todd na waajiri wake kuwahi kuwasilishwa katika wiki 2 zilizopita.
Mashtaka mawili yaliwasililishwa huko nyuma na mwanamke mmoja dhidi ya tabibu Derrick Todd. Moja kati ya mashtaka hayo mawili yanamtuhumu Dakta Todd kwa kuwadhalilisha kijinsia wagonjwa wake.
Wakati huo huo Ingrid Martin Wakili anayemtetea daktari huyo amesema katika taarifa yake ya awali kwamba anaamini kuwa Derrek Todd hajafanya kosa lolote na kwamba atajitetea kwa nguvu zote dhidi ya mashtaka yanayomkabili.
Shtaka la karibuni linaeleza kuwa daktari Todd aliwafanyia wagonjwa wanawake uchunguzi usiofaa ili aweze kuwadhalilisha kingono.