Ujumbe wa maandamano makubwa ya waungaji mkono wa Palestina kimataifa
Zikiwa zimepita wiki tatu tokea kuanza jinai za Wazayuni huko Gaza, uungaji mkono kwa wananchi wa Palestina bado unaendelea kuongezeka katika nchi mbalimbali za Asia na mataifa mengine ulimwenguni.
Kuhusiana na suala hilo makumi ya maelfu ya wananchi wa Malaysia wameshiriki katika maandamano makubwa dhidi ya Wazayuni kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi wa Ghaza ambapo wamepiga nara za kuwaunga mkono wanawake na watoto wasio na ulinzi wa Ghaza. Waandamanaji hao wameelekea katika ubalozi wa Marekani, huku wakilaani vikali utawala wa Kizayuni unaoua watoto na waungaji mkono wake wa Magharibi, ikiwemo Marekani, kwa kutekeleza mauaji ya kimbari huko Ukanda wa Gaza.
Mkutano wa Ukombozi wa Palestina ulioandaliwa na Baraza la Umoja wa Kiislamu nchini Pakistan, umehudhuriwa na wanafikra wa Pakistani, shakhsia wa kidini na Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini humo. Wazungumzaji na Washiriki wa mkutano huo wamesisitiza kuwa, Israel ni utawala haramu na bandia na kuwa njia nzuri zaidi ya kutatua mgogoro Palestina ni kuundwa taifa huru la Palestina. Katika kongomano hilo Nasir Abbas Jafari, Mkuu wa Umoja wa Kiislamu nchini Pakistan amelaani vikali uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Israel, zikiongozwa na Marekani na kushirikiana kwazo na vikosi vinavyoikalia kwa mabavu Al-Quds ambapo amesisitiza kuwa uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani kwa Israel uko wazi na hivyo nchi za Magharibi na hasa Marekani ni wahusika katika mauaji ya Wapalestina. Kwa msingi huo amesema nchi za Kiislamu hazipasi kuzembea katika kukabiliana na hali hiyo kwa shabaha ya kuunga mkono na kuwatetea ndugu zao wa Palestina.
Hii ina maana kwamba Marekani kwa kuzuia kufikishwa misaada ya kibinadamu inashiriki katika mauaji ya halaiki ya Wazayuni huko Ghaza.
Allama Ziaullah Shah Bukhari, kiongozi wa Jamiat Ahl al-Hadith ya Pakistan kwa kutangaza uungaji mkono wake kwa malengo matukufu ya Palestina na kuwaenzi wapiganaji shupavu wa muqawama, amesisitiza kuwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa mbayo ilitekelezwa karibuni na wapiganaji shupavu wa Wapalestina dhidi ya Israel kwa hakika imehuisha mioyo ya mataifa yanayoitetea Palestina na wapenda uhuru wote duniani.
Seyyed Isa Mazari, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Nchi za Kiislamu zina uwezo mkubwa wa kuwazuia Wazayuni na kukomesha jinai zao, na watawala wa nchi za Kiislamu wanapaswa kutekeleza siasa zinazokwenda sambamba na mitazamo ya umma wa Kiislamu katika kuwaunga mkono wananchi wa Ghaza.
Jinai za Wazayuni ni kubwa mno kiasi kwamba hata shakhsia wasiokuwa Waislamu wanazilaani jinai hizo na kuunga mkono wananchi wasio na hatia wa Palestina.
Kimura Mariko, Mkuu wa Ofisi ya al-Quds ya Kituo cha Kimataifa cha Kujitolea cha Japan (JVC), katika mahojiano maalum na shirika la habari la NHK la Japan, amethibitisha mauaji ya raia yanayofanywa kwa makusudi na utawala wa Kizayuni. Katika mawasiliano kwa njia ya video Kimura ambaye hadi sasa yuko Gaza amewakosoa Wazayuni kwa kuendesha mashambulizi ya jinai dhidi ya watu wa Ghaza na kusisitiza kuwa, vikosi vya utawala wa Kizayuni si tu vinalenga Hamas bali pia katika mashambulizi ya karibuni, vimeshambulia pia kambi za wakimbizi huko Gaza.
Katika hali ambayo, kinyume na matarajio ya kimataifa, serikali ya India imesimama upande mwingine kwa kuunga mkono jinai za Wazayuni, wananchi wa India wameunga mkono taifa madhulumu la Palestina kwa kufanya maandamano makubwa katika miji mbalimbali ukiwemo mji wa Kozhikode ulioko kusini mwa nchi hiyo. Katika maandamano hayo makubwa yaliyoandaliwa na Umoja wa Waislamu wa India, makumi ya maelfu ya watu kutoka mji wa Kozhikode,ulioko katika jimbo la Kerala, wametaka kusitishwa vita na kufikishiwa wananchi wa Ghaza misaada ya kibinadamu. Wananchi wa New Delhi, mji mkuu wa India, pia wameitokeza mitaani kufanya maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina, ambapo polisi walizuia kuenea kwake. Hii ni pamoja na ukweli kwamba si tu serikali ya India, bali pia viongozi wengine wanaounga mkono mapatano hawajaweza kuzuia kuenea kuchukizwa wananchi na jinai za Wazayuni.
Nchini Indonesia, ikiwa ni nchi yenye idadi kubwa ya Waislamu duniani, maelfu ya watu wamekusanyika mbele ya ubalozi wa Marekani na kutaka kusitishwa mapigano na mashambulizi ya mabomu huko Gaza. Wakiwa wamevalia nguo nyeupe, waandamanaji hao wamepeperusha bendera za Indonesia na Palestina.
Aidha watu wa Istanbul, Uturuki wamejitokeza mitaani kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Gaza. Maandamano sawa na hayo dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni yamefanyika katika nchi za Denmark, Uingereza, Tunisia na Jordan ambayo yanaonyesha kina cha hasira ya kimataifa dhidi ya Wazayuni. Mohammad Shahada, Mjumbe wa Idara ya Kimataifa ya NHK katika kuelezea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni amewataja wananchi wa Ghaza kuwa madhulumu na kusema kuwa, hata shule zinalengwa na sasa hakuna sehemu salama huko Gaza. Ameendelea kusema kuwa Israel inadai kuwa inalenga Hamas pekee, lakini tumeona majengo ya makazi pia yakilengwa. Shahada amesisitiza kuwa: Huko Gaza, watoto, wanawake na wazee ndio wahanga wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni. Mbali na msaada wa kisiasa na kimaanawi, watu wa Gaza pia wanahitaji misaada mingine kama vile chakula na huduma za afya.
Abdullah Hameed Gul, Mkuu wa Harakati ya Vijana nchini Pakistan, pia anaamini kuhusu suala hilo kuwa Mbali na uungaji mkono wa kisiasa na kidiplomasia kwa Wapalestina, nchi za Kiislamu zinapaswa kufikiria suala la kutoa sio tu mahitaji ya kimsingi kwa wakazi wa Gaza, bali pia silaha na ulinzi kwa wapiganaji wa Muqawama wa Palestina.
Qandeel Abbas, Profesa wa Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Quaid-e-Azam huko Islamabad, pia anasema operesheni ya kishujaa na ya kipekee ya Kimbunga cha Al-Aqsa ni uthibitisho wa kushindwa kwa taasisi za kijasusi na kiusalama za Kizayuni.
Kwa mukhtasari maandamano ya kimataifa ya kuunga mkono Wapalestina yanasisitiza kwamba Suluhu ya mzozo wa Palestina kamwe si kuwepo kwa mataifa mawili, bali maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina ni ya makabila makuu ya dini zote na ni taifa huru la Palestina pekee linalopaswa kuundwa. Ujumbe ambao umekuwa ukiwafikia miaka yote hii viongozi wa utawala ghasibu wa Kizayuni na wala hawana budi ila kuukubali na kuutii.