Maelfu ya Wamarekani waandamana kupinga siasa za Biden
Maelfu ya Wamarekani wamekusanyika mbele ya Ikulu ya White House na New York kupinga siasa za Biden za kuunga mkono jinai za utawala wa kibaguzi wa Israel.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, maelfu ya Wamarekani Ijumaa walimiminika barabarani mjini Washington DC mbele ya Ikulu ya White House na pia katika mji wa New York wakipiga nara za kuunga mkono wananchi wa Palestina na Gaza na kutaka kusitishwa haraka mapigano katika ukanda huo.
Mamia ya wafanyabiashara kote New York pia walikubaliana na wito wa "Funga Biashara kwa ajili ya Palestina", mwishoni mwa juma ili kujiunga na maandamano ya kuunga mkono Palestina.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Novemba 15, 2023, baada ya siku 40 tangu kuanza vita kati ya makundi ya muqawama ya Palestina na utawala wa Israel tarehe 7 Oktoba na kushambuliwa kwa mabomu Ukanda wa Gaza na utawala wa Tel Aviv kwa ajili ya kulipiza kisasi cha operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa na Hamas, lilipasisha azimio likitoa wito wa kusimamishwa vita kwa siku kadhaa kwa jili ya masuala ya kibinadamu.
Azimio hiyo lililopendekezwa na Malta lilipasishwa kwa kura 12 kati ya wanachama 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa bila upinzani au kura ya turufu, lakini wanachama watatu wa kudumu wa Baraza la Usalama, yaani Marekani, Uingereza na Russia, walijiepusha kupigia kura azimio hilo. Marekani na Uingereza zilikataa kupigia kura azimio hilo kwa sababu tu eti Hamas haikulaaniwa, nayo Russia ikakataa kuliunga mkono kutokana na kuwa halikutaka mapigano yasitishwe.
Uungaji mkono wa kiusalama na kijeshi wa nchi za Magharibi hususan Marekani kwa Israel kwa kisingizio cha kujilinda umetoa alama ya kijani kwa utawala huo kuendelea kuwaua kikatili watoto na wanawake wa Kipalestina.