Kufukuzwa Manowari ya Marekani kutoka kwenye maji ya China
(last modified Mon, 27 Nov 2023 02:44:00 GMT )
Nov 27, 2023 02:44 UTC
  • Kufukuzwa Manowari ya Marekani kutoka kwenye maji ya China

Ingawa muda mrefu haujapita tangu kufanyika kikao kati ya marais wa Marekani na China mjini San Francisco, kikao ambacho Rais Joe Biden wa Marekani alikitaja kuwa chanya, Tian Junli, Msemaji wa Kamandi ya Pamoja ya Vikosi vitatu vya Jeshi la Nchi Kavu, Anga na Baharini vya Jeshi la China ametangaza kufukuzwa manowari ya Marekani kutoka kwenye eneo la maji ya nchi hiyo.

Haionekani kuwa manowari hiyo ya Marekani ameingia kwa makosa na bila kukusudia katika maji ya China, na kuna uwezekano mkubwa kwamba hatua hiyo ni katika mwendelezo wa chokochoko za Marekani dhidi ya China.

Ni kutokana na uwezekano huo ndipo Jeshi la Wanamaji la China likaamua kuifukuza manowari hiyo kwa jina la USS Hopper iliyo na uwezo wa kurusha makombora yanayoelekezwa kutokea mbali, baada ya kuingia kinyume cha sheria kwenye maji ya China karibu na Visiwa vya Shisha katika Bahari ya Kusini ya China. Tangu kipindi cha urais wa Barack Obama huko Marekani, sio tu kwamba Marekani imekuwa ikilenga kuidhibiti China, bali Jeshi la Wanamaji la Merekani limeongeza uwepo wake katika Bahari ya China Kusini na pia kufanya mazoezi na washirika wake kama Japan, Korea Kusini na Ufilipino. Kwa hivyo, inaonekana kuwa Marekani inakiuka kwa makusudi mamlaka ya China kwa lengo la kuendelea kuvuruga hali ya usalama ya Asia Mashariki.

Lu Chao, mtaalamu wa masuala ya Peninsula ya Korea na Asia ya Mashariki katika Chuo Kikuu cha Taaluma ya Jamii cha Liaoning, anasema kuhusu suala hili: "Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imeongeza harakati zake za kichochezi katika maji yanayoizunguka China na kujitahidi kujenga ushirikiano wa kijeshi na nchi za eneo ili kuongeza mashinikizo dhidi ya China. Hii ni katika hali ambayo washirika wa Washington, ikiwa ni pamoja na Korea Kusini, wanapaswa kuwa waangalifu na kutoingilia mambo ya ndani ya China.

Kwa mujibu wa tangazo la kamandi ya pamoja ya vikosi vitatu vya jeshi la China, Marekani imehatarisha sana mamlaka na usalama wa China kwa kuelekeza manowari yake kwenye maji ya China, suala ambalo ni uthibitisho wa wazi kwamba Washington inataka kufanya maji ya Bahari ya Kusini ya China kuwa eneo la harakati za kijeshi.

Manowari ya USS Hopper

Kwa hiyo, hatua ya jeshi la China ya kuifukuza mara moja manowari ya Marekani mara tu baada ya kuingia katika eneo la maji yake inaonyesha aina fulani ya utunishaji misuli na kudhihirisha nguvu zake dhidi ya uchochezi wa adui. Ikiwa lengo la Marekani ni kupima kiwango cha utayari na umakini wa jeshi la China, basi kufukuzwa mara moja manowari yake kutoka kwenye eneo la maji ya China linaweza kuwa onyo la wazi kwa Ikulu ya White House. Ashley Van Tee mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema:

Uwepo wa kudumu wa meli za kivita za Marekani katika maji ya Bahari ya Kusini ya China, pamoja na mazoezi ya mara kwa mara ya majini na Ufilipino, Korea Kusini, Japan na hata Australia, kumepelekea China kuweka jeshi lake, hasa jeshi la wanamaji, katika hali ya tahadhari kamili na tukio la karibuni la kukabiliana mara moja na manowari ya Marekani na kufukuzwa kutoka kwenye eneo la maji ya China kunathibitisha wazi suala hilo.

Kwa vyovyote vile, taarifa ya kamandi ya pamoja ya vikosi vitatu vya jeshi la China katika eneo la kusini imesisitiza kuwa jeshi la wanamaji na anga la China limetumwa katika eneo la Bahari ya Kusini ya China kufuatilia na kuonya meli za wavamizi katika maji hayo na kuwa limewekwa katika hali ya tahadhari na kupewa ruhusa ya kuchukua hatua zozote kwa ajili ya kulinda mamlaka na ardhi yote ya China, usalama wa eneo, amani na utulivu. Ni wazi kuwa Marekani inajaribu kupuuza maonyo hayo ya China na kuendelea kujaribu kuvuruga uthabiti na usalama wa eneo hilo hasa katika Bahari ya Kusini ya China.

Wakati huo huo, Henry Kissinger, mtaalamu wa ngazi za juu wa masuala ya kimataifa, amekuwa akiionya Ikulu ya White House kila mara kwamba masuala ya ardhi ni mstari mwekundu wa Beijing, na kuwa iwapo Washington itapuuza suala hilo, itasababisha mgogoro na vita.