US yaendelea kuwawekea mbinyo wanachuo wanaoitetea Palestina
Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani kimewasimamisha masomo zaidi ya wanafunzi 65 kufuatia maandamano yao ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina ambayo yalitokea kwenye Maktaba ya Butler.
Hali kadhalika maandamano hayo ya Jumatano yalipelekea watu zaidi ya 80 kukamatwa, maafisa wa chuo kikuu walithibitisha hayo jana Ijumaa.
Kwa mujibu wa msemaji wa chuo kikuu hicho, wanafunzi 65 zaidi waliohusika katika maandamano hayo sasa "wamesimamishwa (masomo) kwa muda" huku uchunguzi ukiendelea.
Wakati huo huo, watu wasiopungua 33 kutoka vyuo tanzu wamezuiwa kutoka kwenye kampasi ya Morningside Heights. Aidha wahitimu walioshiriki maandamano hayo wamezuiwa kurejea chuoni.
Washiriki wa maandamano hayo wamebainisha wasi wasi wao kuhusiana na vita vya Israel dhidi ya Gaza ambavyo hadi sasa vimegharimu maisha ya takriban Wapalestina 52,800, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Pia wameshutumu uungaji mkono usioyumba wa Marekani kwa Israel, na kuikosoa Washington kwa kuunga mkono vita hivyo kwa njia ya usaidizi wa kijeshi na ufadhili wa kisiasa.
Wanachuo wanaoandamana na kukusanyika kwenye kampasi za vyuo vikuu vyao wanautaka uongozi wa vyuo ukate uhusiano na Israel, ambayo baadhi ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema inafanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.