Maandamano ya kuwaunga mkono Wagaza yafanyika Iran, Yemen
Maelfu ya watu walimiminika barabarani na mitaani katika miji yote ya Iran baada ya Swala ya Ijumaa kushiriki maandamano ya kitaifa ya "Ijumaa ya Ghadhabu", wakitangaza uungaji mkono wao usioyumba kwa Wapalestina wa Gaza, na kulaani mauaji ya kimbari ya Israel katika eneo hilo lililozingirwa.
Mbali na mji mkuu Tehran, maandamano hayo yalifanyika kwa wakati mmoja katika miji mbali mbali ya Iran. Washiriki wa maandamano hayo walibeba mabango yenye jumbe za kulaani jinai za Israel, huku wakipiga nara tofauti kama "Mauti kwa Marekani" na "Mauti kwa Israel."
Maandamano hayo yamedhihirisha hasira za wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu juu ya mauaji ya kimbari yanayofanywa na Wazayuni huko Gaza.
Aidha maandamano hayo yameonyesha namna wananchi wa Iran walivyofungamana na mrengo wa Muqawama wa Wapalestina.
Wakati huo huo, wananchi wa Yemen katika mji wa Saada pamoja na miji mingine ya nchi hiyo, jana pia walifanya maandamano makubwa ya kuiunga mkono Palestina sanjari na kulaani vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Waandamanaji walitangaza kuunga mkono Wapalestina huko Gaza, huku wakilaani na kukosoa uhalifu wa kivita wa Israel kwa ushirikiano wa Marekani. Aidha walipeperusha bendera za Palestina na kubeba picha za watoto waliouawa shahidi katika mashambulizi ya anga ya Israel huko Gaza.
Maandamano hayo yamejiri baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kutoa wito kwa Wapalestina, Waarabu, Waislamu na watu huru kote duniani kushiriki katika harakati ya kimataifa na maandamano ya 'ghadhabu za kimataifa' kuadhimisha siku 600 za "mauaji ya halaiki na njaa" dhidi ya watu wa Gaza.
Israel ilianzisha mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023. Tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina 54,000 wameuawa shahidi, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.