Iran yakanusha taarifa za kukaribia makubaliano na Marekani
(last modified Fri, 30 May 2025 07:35:36 GMT )
May 30, 2025 07:35 UTC
  • Iran yakanusha taarifa za kukaribia makubaliano na Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesisitiza dhamira ya Tehran ya kuendelea kushiriki katika mchakato wa kidiplomasia, huku akilaani kile alichokieleza kuwa ni upotoshaji wa vyombo vya habari unaolenga kuvuruga mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea kati ya Iran na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii X siku ya Alhamisi, Araghchi amejibu tetesi zinazoenea kwenye vyombo vya habari kuhusu uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano ya haraka kati ya Iran na Marekani.

Amesema: “Vyombo vya habari vinaeneza tetesi kuhusu makubaliano ya karibu kati ya Iran na Marekani. Hatuwezi kusema tupo hapo bado. Iran ina nia ya dhati ya kufikia suluhisho la kidiplomasia ambalo litazingatia maslahi ya pande zote. Lakini hilo linawezekana tu kwa makubaliano yatakayohakikisha kuondolewa kwa vikwazo vyote na kuheshimu haki za nyuklia za Iran—ikiwemo uwezo wa kurutubisha urani.”

Akijibu taarifa ya kituo cha FOX News cha Marekani, Araghchi amesisitiza kuwa mafanikio ya maana yanaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo, na si kwa matamko ya vyombo vya habari,

Kwa mujibu wa FOX News, ripoti mpya ya kiintelijensia imeibua madai kuwa Iran inaendelea na mpango wake wa silaha za nyuklia na kwamba mpango huo unaweza kutumika kurusha makombora ya masafa marefu.

Hata hivyo, FOX News imekiri kuwa kile kilichoelezwa kuwa ni taarifa mpya kinakinzana na kauli ya Mkurugenzi wa Kitaifa wa Ujasusi wa Marekani, Tulsi Gabbard, aliyeiambia Kamati ya Seneti ya Usalama wa Taifa mwezi Machi kuwa mashirika ya kiintelijensia ya Marekani “yanaendelea kutathmini kuwa Iran haitengenezi silaha za nyuklia.”

Araghchi pia amekemea kile alichokitaja kuwa ni upotoshaji unaolenga kuvuruga juhudi za kidiplomasia, akiikosoa Israel kwa kutumia jina la Iran kama njia ya kuwavunjia heshima wakosoaji wa Marekani. Amesema kuwa mbinu hizo ni za kiwango cha chini hata kwa vigezo vya Israel, na zinaweza kudhoofisha juhudi za kweli za kutafuta suluhu kwa njia ya mazungumzo.

Iran na Marekani tayari zimefanya duru tano za mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja tangu Aprili 12, na pande hizo mbili zinatarajiwa kukutana tena kwa ajili ya majadiliano yenye lengo la kufikia makubaliano mapya. Hata hivyo, mvutano bado upo kuhusu kiwango cha urutubishaji wa madini ya urani.

Rais wa Marekani, Donald Trump, siku ya Jumatano alisema kuwa amemuonya binafsi Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kutovuruga mazungumzo hayo.