WHO: Matumizi ya tumbaku yanaua watu milioni 6 kila mwaka
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, matumizi ya tumbaku huua takribani watu milioni sita kila mwaka. Watu laki sita kati ya hao, hufa kutokana na kuathiriwa na moshi wa sigara zinazovutwa na watu wengine.
Katika taarifa iliyotolewa kwa mnasaba wa Siku ya Dunia Bila ya Tumbaku inayoadhimishwa leo, na ambayo huadhimishwa tarehe 31 Mei kila mwaka na ambayo inajuulikana pia kama Siku ya Kupambana na Matumizi ya Tumbaku imeelezwa kuwa, kuuna haja ya kuchukuliwa hatua zaidi za kuwaelimisha watu madhara ya matumizi ya tumbaku.
Nchi Wanachama wa Shirika la Afya Ulimwenguni ziliunda Siku ya Kupinga Matumizi ya Tumbaku Duniani mwaka 1987 ili kueleza janga la tumbaku, vifo vinavyoweza kuzuilika na magonjwa yanayosababishwa na tumbaku.
Matumizi ya tumbaku, haswa kupitia sigara, yana athari mbaya kwa mwili - hudhuru karibu kila kiungo katika mwili, na uvutaji sigara ni moja ya sababu kuu ya vifo vya mapema.
Inakadiriwa kuwa kufikia mwaka 2030 watu milioni nane watakuwa wanakufa kwa sababu ya tumbaku, kwa mujibu kwa Taasisi ya Saratani ya Marekani (ACS). Katika nchi ya Marekani pekee, uvutaji sigara husababisha vifo vya watu 480,000 kila mwaka.
Matumizi ya tumbaku barani Afrika yana athari mbaya kiafya, kimazingira na kiuchumi. Kwa upande wa afya, ni chanzo kikuu cha vifo vinavyoweza kuzuilika, kutokana na magonjwa mbalimbali ya saratani, magonjwa ya moyo na mapafu. Kimazingira, kilimo cha tumbaku kinaweza kusababisha ukataji miti na uharibifu wa udongo. Kiuchumi, matumizi ya tumbaku huelemea mifumo ya afya kama hospitali.