Russia: Wamagharibi hatimaye wataondoka Ukraine
Mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Kigeni ya Russia amesema: "Utawala kibaraka wa Kyiv, ambao ni ngeni kwa watu wengi wa Ukraine na umetekeleza mauaji ya umwagaji damu huko Donbass, Odessa na miji na vijiji vingi vya nchi hiyo, hatimaye utaachwa na kutupiliwa mbali na Wamagharibi."
Sergey Naryshkin amesema kwamba nchi za Ulaya na Marekani tayari zinatafuta mbadala za Rais wa sasa wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, na kwamba moja ya sababu za hatua hiyo ni kiburi cha Zelenskyy na kupenda jaha na makuu kusikokuwa na mwisho kwa kiongozi huyo.
Sergey Naryshkin pia amesema kuwa sababu nyingine za uamuzi huo wa nchi za Magharibi ni pamoja na ahadi za Zelenskyy ambazo hazijatekelezwa, kupoteza uwezo wake wa kuongoza vita vya Ukraine, upendeleo na ufisadi usio na mipaka nchini Ukraine ambao ukubwa wake umewashtua hata wanasiasa wa Magharibi.
Vita vya Ukraine na athari zake mbaya za kisiasa, kijeshi, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni viko katika mwezi wa 22, na nchi za Magharibi bado zinatuma silaha kwa serikali ya Kyiv.
Maafisa wa serikali ya Russia na baadhi ya wataalamu na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi wamevitaja vita vya Ukraine kuwa ni vita vya niaba kati ya Magharibi na Russia.