Jan 08, 2024 06:39 UTC
  • China yayawekea vikwazo makampuni matano ya Marekani kwa kuiuzia silaha Taiwan

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imetangaza vikwazo dhidi ya makampuni matano ya Marekani kwa kuiuzia Taiwan silaha.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilitangaza Jumapili kwamba imeyawekea vikwazo makampuni matano ya masuala ya ulinzi ya Marekani ukiwa ni mjibizo kwa hatua yao ya kuiuzia silaha Taiwan na hatua ya Washington ya kuyawekea vikwazo makampuni na watu binafsi wa China.
Maafisa wa China wanaichukulia Taiwan kuwa sehemu isiyoweza kutenganishwa ya ardhi ya nchi hiyo na daima wamekuwa wakionya dhidi ya hatua za Marekani zinazosababisha mvutano za kuiuzia Taiwan silaha.
China inachukulia hatua ya Marekani ya kuiuzia Taiwan silaha kuwa ni kuingilia masuala yake ya ndani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imetangaza kuwa kwa mujibu wa vikwazo vipya vya China, mali zote za makampuni hayo matano ya Marekani nchini China zitazuiliwa, na mashirika na watu binafsi nchini China watapigwa marufuku kufanya biashara na miamala yoyote na makampuni hayo matano.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imetangaza pia kwamba hatua za Marekani zinadhoofisha mamlaka na maslahi ya usalama ya China, zinayumbisha amani na utulivu katika eneo la Mlango-Bahari wa Taiwan, na zinakiuka pia haki na maslahi ya makampuni na watu binafsi wa China.

Mwezi uliopita (Desemba 2023) Marekani iliidhinisha mauzo ya vifaa vya mawasiliano na ulinzi kwa Taiwan vyenye thamani ya takriban dola milioni 300, hatua ambayo ilikosolewa na China.../

Tags