Jan 10, 2024 06:19 UTC
  • China yaijuza Marekani kwamba 'haitalegeza msimamo katu' juu ya Taiwan

China imeapa kutekeleza bila kuyumbayumba msimamo wake wa kuiunganisha tena Taiwan na ardhi kuu ya nchi hiyo na kuitaka Marekani iache kukipatia silaha kisiwa hicho na kupunguza harakati zake katika Bahari ya China Kusini.

Taarifa iliyotolewa leo na wizara ya ulinzi ya China imesema, maafisa wa jeshi la China wamewaambia wenzao wa Marekani kwenye mazungumzo yaliyofanyika wiki hii kwamba Beijing "haitakubali kamwe" kulegeza msimamo kuhusu suala la Taiwan na kuwataka waache "vitendo vya uchochezi" katika Bahari ya Kusini ya China.

Wizara hiyo imeeleza katika taarifa hiyo iliyotoa ufafanuzi wa yaliyojiri katika mazungumzo yaliyofanyika siku ya Jumatatu na Jumanne baina ya maafisa wa kijeshi wa Beijing na Washington kwamba, China "imesisitiza kuwa haitakubali kamwe kufikia maelewano au kulegeza msimamo juu ya suala la Taiwan," na imeitaka Marekani "ikome kukipa silaha" kisiwa hicho kinachojiendeshea mambo yake ambacho kitakuwa na uchaguzi wiki hii.

Taarifa ya wizara ya ulinzi ya China imefafanua kuwa katika mazungumzo hayo Beijing imebainisha nia yake ya kuendeleza uhusiano mzuri na thabiti wa kijeshi na Marekani kwa msingi wa usawa na kuheshimiana.

Rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa China Xi Jinping walikubaliana mwezi Novemba kuanzisha upya mazungumzo muhimu ya kijeshi kati ya nchi hizo, yaliyositishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Kwa mujibu wa duru za Washington, mazungumzo ya wiki hii ambayo yalifanyika katika wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, yaliongozwa na naibu waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Michael Chase na ujumbe wa China uliongozwa na Meja Jenerali Song Yanchao.../

Tags