Jan 22, 2024 08:50 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Jan 22

Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa.

Kombe la Asia; Iran yailaza Hong Kong

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendelea kung'ara katika michuano ya fainali za Kombe la Asia nchini Qatar. Siku ya Ijumaa, Team Melli kama inavyofahamika hapa nchini, iliizaba Hong Kong bao moja bila jibu katikak mchuano wake wa pili wa Kndi C uliopigwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa huko al-Rayyan nchini Qatar. Bao la pekee la mechi hiyo na la ushindi kwa Iran lilitiwa kimyani na Mehdi Qaedi katika kipindi cha kwanza. Kabla ya hapo, Iran ilifanikiwa kuichabanga Palestina mabao 4-1 katika mchezo wa ufunguzi uliopigwa katika Uwanja wa Jiji la Elimu huko al-Rayyan nchini Qatar. Iran inasalia kileleni mwa Kundi C ikiwa na alama 6 na sasa imejiunga na mwenyeji Qatar, Australia na Iraq kaktika raundi ya 16. Vijana hao wa Kiirani wanaonolewa na Amir Ghalenoei wamepangwa katika Kundi C pamoja na Imarati, Palestina na Hong Kong kwenye michuano hiyo ya kibara iliyong'oa nanga Ijumaa huko Doha. Team Melli ya Iran ambayo inapania kuhitimisha ukame wa miaka 47 wa kutwaa taji hilo la kieneo, inatazamiwa kushuka dimbani kuvaana na Imarati Jumanne hii ya Januari 23.

Basketboli ya walemavu; Iran ya Pili

Timu ya mpira wa kikapu ya walemavu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili katika mashindano ya kieneo ya basketboli ya eneo la Asia Oceania ya mwaka huu 2024. Iran ilishindwa kufurukuta katika fainali iliyopigwa Jumamosi huko Bangkok, mji mkuu wa Thailand na kukubali kichapo cha vikapu 53-51. Kabla ya hapo pia, Iran ilibamizwa vikapu 69-60 na Australia. Hata hivyo katika mechi zake za awali, Iran ilizitandika Korea Kusini, Thailand, Japan, China na Afghanistan na kufanikiwa kutinga fainali.

Timu ya basketboli ya viti vya magurudumu (viti vya mwendo)

Korea Kusini imetunikiwa medali ya shaba baada ya kuibuka kidedea katika mchuano wa kutafuta mshindi wa tatu ilipovaana na Japan. Timu ya basketboli ya viti vya magurudumu (viti vya mwendo) ya Iran hivi majuzi iliteuliwa kuwa timu bora ya Asia na Kamati ya Paralimpiki ya Asia. Mashindano hayo ya walemavu ya Asia Oceania Championships yamefanyika Bangkok, mji mkuu wa Thailand kuanzia Januari 12 hadi 20.

Michuano ya AFCON; miamba yatikiswa

Tuangazie matokeo ya baadhi ya mechi za duru ya 34 ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON zinazoendelea kuroroma nchini Ivory Coast. Bao la dakika za mwisho kutoka kwa Baghdad Bounedjah liliwazolea miamba ya soka ya Afrika, Algeria pointi ya pili katika Kundi D kwenye fainali za Kombe la Afrika (Afcon) baada ya kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya Burkina Faso. Mohamed Konate aliwaweka Burkina Faso almaarufu Stallions kifua mbele mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya juhudi zake kufutwa na Bounedjah aliyesawazisha mambo mwanzoni mwa kipindi cha pili. Ingawa Bertrand Traore alirejesha Burkina Faso uongozini kupitia penalti ya dakika ya 71, Algeria ambao ni wafalme mara mbili wa Afcon walijituma maradufu hadi wakaondoka uwanjani na alama moja muhimu. Matokeo hayo yameiacha Burkina Faso na alama nne sawa na Angola walioipepeta Mauritania mabao 3-2 katika pambano jingine la Kundi D, Jumamosi. Huku hayo yakiarifiwa, Tiago Manuel Bebe alifunga mkwaju wa ikabu kutoka hatua ya 40 na kuongoza Cape Verde kuigaragaza Msumbiji mabao 3-0 katika mchuano wa pili wa Kundi B kwenye fainali hizo za AFCON nchini Ivory Coast. Nahodha Ryan Mendes alipachika wavuni bao la pili baada ya kumuacha hoi kipa Ernan Siluane aliyezidiwa pia maarifa na Kevin Pina. Ushindi wa Cape Verde uliwapa uhakika wa kumaliza kampeni za Kundi B kileleni mbele ya mabingwa wa zamani Misri na Ghana.

 

Wakati huohuo, mabingwa watetezi wa Kombe la Afrika (Afcon), Senegal, walijikatia tiketi ya hatua ya 16-bora baada ya kuisasambua Cameroon mabao 3-1 katika ‘Kundi C’ uwanjani Charles Konan Banny jijini Yamoussoukro mnamo Ijumaa. Ismaila Sarr aliwaweka Senegal kifua mbele kunako dakika ya 16 kabla ya Habib Diallo kufanya mambo kuwa 2-0 katikati ya kipindi cha pili. Ingawa Jean-Charles Castelletto alirejesha Cameroon mchezoni katika dakika ya 83, lakini nyota Sadio Mane aliifungia Senegal bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya George-Kevin Nkoudou kupoteza nafasi ya kusawazisha. Siku ya Jumapili Afrika Kusini iliifanyia vibaya Namibia, kwa kuicharaza kimwizi mabao 4-0.

Aidha siku ya Jumapili, mwakilishi wa Afrika Mashariki kwenye fainali hizo, Taifa Stars ya Tanzania waliambulia sare ya bao 1-1 walipovaana na Zambia katika Uwanja wa Stade de San Pedro. Vijana wa nyumbani walitangulia kuona nyavu za Wazambia kupitia goli la mapema la Simon Msuva.

Rais wa TFF, Wallace Karia

 

Hata hivyo Zambia walijizoazoa na kufanya mambo kuwa sawa bin sawa kunako dakika ya 88, kupitia kombora la Patson Daka. Ikumbukwe kuwa, Kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka barani Afrika CAF imemfungia kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Adel Amrouche mechi 8 kwa kutoa kauli ambazo zimetafsiriwa kama ni kauli za uchochezi. Siku moja kabla ya mchezo wa kwanza dhidi ya Morocco, kocha Adel aliwatuhumu Morocco kwamba wao ndio wanaouendesha mpira wa Afrika kwa kuamua wacheze muda gani, waamuzi wa mechi zao na kupanga ratiba za michezo yao. Kauli hiyo ilikanushwa na TFF kupitia Rais Wallace Karia ambaye alisisitiza kuwa kauli hiyo ni ya kocha binafsi na sio ya TFF. TFF tayari imechukua hatua ya kumsimamisha Amrouche, na sasa joho lake linavaliwa na Hemed Moroko akisaidiwa na Juma Mgunda.

Morocco ambayo iliigaragaza Tanzania mabao 3-0, siku ya Jumapili ilitolewa kijesho na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na DRC. Waarabu hao walikuwa wametanguliwa kuona nyavu kwa goli la Achraf Hakimi, lakini Silas Katompa Mvumpa akawasawazishia batoto la Kongo.

Ligi ya EPL

Klabu ya Arsenal wamefufua matumaini ya kusalia miongoni mwa wagombezi halisi wa taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu wa 2023-24 baada ya kuiponda Crystal Palace mabao 5-0 uwanjani Emirates. Vijana hao wa kocha Mikel Arteta walishuka dimbani Jumamosi wakiwa na presha kali ya kujinyanyua baada ya kupoteza mechi tatu kati ya tano katika EPL mwishoni mwa mwaka wa 2023. Wakicheza dhidi ya Palace, walikamilisha kipindi cha kwanza wakivuna uongozi wa mabao 2-0 kupitia bao la Gabriel Magalhaes aliyefunga kwa kichwa na la kipa Dean Henderson aliyejifunga kutokana na mpira wa kona.

 

Fowadi wa zamani wa Brighton, Leandro Trossard, aliwafungia Gunners goli la tatu kabla ya Gabriel Martinelli kutokea benchi katika kipindi cha pili na kucheka na nyavu za Palace mara mbili. Arsenal sasa wapo katika nafasi ya tatu katika jedwali la EPL wakiwa na alama 43 sawa na Aston Villa na mabingwa watetezi Manchester City, ambao wikendi waliizaba New Castle mabao 3-2.

Liverpool wametuama kileleni mwa jedwali wakiwa na alama 48. Wikendi Liverpool waliionyoa bila maji Bournmouth kwa kuichabanga mabao 4-0. Mashteni Wekundu hawana mpya, Jumapili walilazimishwa sare ya mabao 2-2 walipochuana na Tottenham.

………………….TAMATI...…………..

 

Tags