Ulimwengu wa Spoti, Apr 21
(last modified Mon, 21 Apr 2025 07:11:47 GMT )
Apr 21, 2025 07:11 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Apr 21

Hujambo mskilizaji wa RT na hasa ashiki na mfuatiliaji wa masuala ya spoti. Karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika kona mbali mbali za dunia.....

Wanamichezo bingwa wa Iran watuzwa

Siku ya Jumatano, Mehdi Taremi, mshambuliaji nyota wa timu ya taifa ya kandanda ya Iran na klabu ya Inter Milan ya Italia, pamoja na Nahid Kiani, bingwa wa taekwondo na mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki, walitunukiwa tuzo za juu katika sherehe za kila mwaka za tuzo za michezo hapa Tehran. Wakati Taremi akiondoka na tuzo ya ‘Mwanamichezo wa Kiume wa Mwaka wa Kiiarani wa 1403 uliomalizika Machi 21, 2025’, Kiani alinyakua tuzo ya ‘Mwanariadha Bora wa Kike wa Mwaka 1403’ katika kura zilizopigwa na wananchi kote nchini.

 

Sherehe za kufunga duru ya nne ya 'Sherehe za Mabingwa wa Iran' zilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha IRIB, na kuhudhuriwa na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, Waziri wa Michezo na Vijana, Ahmad Donyamali na Mkuu wa shirika la utangazaji la Iran IRIB, Peyman Jebelli. Katika hafla hiyo pia walikuwamo maafisa wakuu wa Kamati za Kitaifa za Olimpiki na Michezo ya Walemavu, wakuu wa mashirikisho mbalimbali ya michezo, pamoja na wanariadha na  wanamichezo mashuhuri wa Iran. Hafla hizo za utoaji tuzo zilizozinduliwa mwaka wa 2021 na Idhaa ya Michezo ya IRIB, ni mpango unaolenga kuwatuza na kuwaenzi wanamichezo na wanariadha hapa nchini. Tangu wakati huo, tamasha hilo limekuwa likifanyika kila mwaka kwa lengo la kuimarisha fahari ya taifa, kuonesha mafanikio ya kimichezo, na kuheshimu na kuenzi juhudi za mabingwa wa Iran.

Wanariadha wa Iran wazoa medali

Wanaridha wa kike wa Iran, Samia Shahpari na Amirreza Ahanin Maram wa Iran wameshinda medali katika Mashindano ya 6 ya Riadha ya Asia ya Vijana wenye chini ya miaka 18. Shahpari alitwaa nafasi ya tatu katika mbio za mita 3000 za Wanawake kwa kutumia muda wa dakika 10:09.07. Medali ya dhahabu ilimwendea Anastasiya Silchenkova wa Uzbekistan, ambaye alikata utepe wa ushindi kwa kutumia dakika 9:45.17, huku Mchina Suolang Zhuoma akitwaa fedha kwa muda wa dakika 10:00.44. Hapo awali, Ahanin Maram alipata medali ya fedha katika Mchezo wa Kurusha Kitufe kwa Wanaume wenye chini ya miaka 18, ambapo alikitupa umbali wa mita 71.05. Medali ya dhahabu ilitwaliwa na Mohammed Siraj Alzayer wa Saudi Arabia, alikiyerusha umbali wa mita 72.91, huku shaba ikimuendeaWang Ankang wa China kwa kukitupa mita 70.72. Mashindano ya Riadha ya Asia U18 2025 yalifanyika katika Jiji la Mwanamfalme Nayef huko Qatif, Saudi Arabia, kuanzia Aprili 15 hadi 18.

Basketboli: Wanawake wa Iran wasonga mbele

Timu ya mpira wa kikapu ya wanawake ya Iran iliichabanga Jordan vikapu 88-70 katika Divisheni B ya Kombe la Asia la Wanawake la FIBA 2025. Timu hiyo ya Iran almarufu Banovan ilikuwa imeishinda Syria 66-55 Jumanne usiku. Kwa ushindi huo, Iran imefuzu Divisheni B ya Kombe la Asia la FIBA ​​la Wanawake la 2025. Mashindano hayo ya kieneo wa mpira wa kikapu ya wanawake yalifanyika Amman, mji mkuu Jordan.

Magongo ya theluji; Iran ya 5

Iran ilishindwa na Kuwait alama 11-0 (2–0, 5-0, 4-0) katika Divisheni ya Nne ya Dunia ya IIHF ya 2025 siku ya Jumamosi na kumaliza katika nafasi ya tano kwa pointi tatu pekee katika michuano hiyo yenye timu sita.  Timu Melli kama inavyofahamika hapa nchini, hapo awali ilipoteza dhidi ya Indonesia 2-1, Uzbekistan 20-0, na Armenia 8-0 na kuishinda Malaysia 5-1. Mashindano hayo yalifanyika Yerevan, Armenia, kuanzia Aprili 13 hadi 19. 

Simba yasonga mbele kwa madaha

Klabu ya soka ya Simba ya Tanzania imejiweka katika mazingira mazuri baada ya kuvuna ushindi japo lani kwenye mchezo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya klabu ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini uliopigwa wikendi. Katika mchezo hu uliopigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 mfungaji akiwa Jean Charles Ahoua katika dakika za majeruhi kabla ya kumaizika kipindi cha kwanza. Kutokana na matokeo hayo, Wekundu wa Msimbazi sasa wanahitaji sare ya aina yoyote katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Aprili 27 nchini Afrika Kusini, ili itinge hatua ya fainali ya michuano hiyo. RAIS wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, ameipongeza timu ya Simba ya Dar es Salaam kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini, mmchezo kwa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika uliofanyika Uwanja wa New Amaan Complex. “Hongera sana kwa Klabu ya Simba kwa ushindi katika mchezo wa Mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF Confederation Cup). Mmeleta furaha kwa mashabiki wenu na Watanzania wote na kuipeperusha vyema bendera ya nchi yetu. Motisha kutoka kwangu mtaipokea kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Ninawatakia kila la kheri,” ameandika Rais Samia kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii. Hebu sikiliza mikogo na mbwembwe za mashabiki, wachezaji na wasimamizi wa Simba kufuatia ushindi huo.

Mashabiki wa Simba washangilia bao

 

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imetoa adhabu kali kwa timu za MC Alger na Esperance kutokana na vurugu za mashabiki, wachezaji na maofisa wao ugenini katika mechi za hatua ya robo fainali dhidi ya Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns. Kamati ya nidhamu ya CAF, imeitoza MC Alger faini ya fedha kiasi cha Dola 100,000 kwa kosa la vurugu ambazo timu na mashabiki wake walifanya dhidi ya Orlando Pirates kwenye Uwanja wa Orlando, Johannesburg, Aprili 9 mwaka huu. Kocha msaidizi wa MC Alger, Mohamed Khezrouni amepewa adhabu ya kufungiwa michezo minne ya CAF huku beki wake Abdelkader Oussama Menezia akifungiwa mechi mbili. Esperance nayo imetozwa kiasi cha Dola 100,000 kwa kosa la vurugu ambazo mashabiki wake walifanya Aprili Mosi mwaka huu dhidi ya Mamelodi Sundowns katika Uwanja wa Loftus Versfeld. Katika mchezo huo, Mamelodi Sundowns iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Peter Shalulile. Mamelodi Sundowns ilifanikiwa kusonga mbele kwa ushindi wa bao 1-0 kwani mechi ya marudiano Tunisia, timu hizo zilitoka sare tasa. Orlando Pirates nayo ilitoka sare ya bila kufungana katika mechi hiyo ya Aprili 9 nyumbani lakini ikasonga mbele kwa vile iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini, Aprili Mosi. Hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu itahusisha Mamelodi Sundowns itakayocheza na Al Ahly na Orlando Pirates itakayocheza na Pyramids FC.

Deby ya Kariakoo yamuibua Waziri Kabudi

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tz, Profesa Palamagamba Kabudi, amewataka mashabiki wa soka nchini humo kuwa na subira kuhusu sakata la kutochezwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba SC na Yanga SC, maarufu kama Dabi ya Kariakoo. Waziri Kabudi alieleza hayo Aprili 14 jijini Dodoma kuwa mamlaka husika, ambazo ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ndizo zenye mamlaka ya kutoa taarifa rasmi kuhusu hatma ya mchezo huo. Mchezo huo, uliopangwa kufanyika Machi 8, 2025, uliahirishwa kutokana na mvutano kati ya klabu hizo mbili. Simba SC ilidai kuwa haikuruhusiwa kufanya mazoezi ya awali uwanjani na hivyo kuamua kutoshiriki mchezo huo, wakati Yanga SC ilisisitiza kuwa mchezo huo ungechezwa kama ulivyopangwa. Baadaye, Bodi ya Ligi iliahirisha rasmi mchezo huo, ikitaja sababu za kiusalama na mazingira ya dharura.

Starlets ya Kenya walimwa na Cameroon

Mbali na hayo, mabanati wa Kenya walipokea kichapo chembamba cha bao 1-0 kutoka kwa Cameroon katika mchujo wa mwisho wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake Wenye Chini ya Miaka 17. Wasichana hao wa Kenya walishindwa kurufukuta katika mchuano huo wa Jumapili, Aprili 20, licha kuupigia nyumbani katika kwenye Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi. Starlets ilitawala hatua za mwanzo, ikitengeneza nafasi kadhaa mashuhuri. Hata hivyo, Cameroon walitumia nafasi yao katika dakika ya 30 pale Melong alipoinuka kwa kichwa akiunganisha kona iliyopigwa na Ngassa Yolande, na kuwapa wageni uongozi muhimu. Kupoteza huku kunaweka shinikizo kubwa kwa Junior Starlets kabla ya mechi ya mkondo wa pili huko Yaoundé baadaye mwezi huu. Starlets wanakabiliwa na kibarua kigumu cha ugenini Aprili 25 huko Stade Olembe mjini Yaoundé, ambapo ushindi ni muhimu ili kuweka hai matumaini ya kucheza kwa mara ya pili kwenye Kombe la Dunia la FIFA la Wanawake U17. Mashindano ya mwaka huu, toleo la tisa, yataandaliwa na Morocco kuanzia Oktoba 7 hadi Novemba 8, 2025.

UEFA; Arsenal yatinga nusu fainali kwa madaha

Klabu ya Arsenal imeandika historia tena baada ya kufuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya tatu katika historia yake. Hii ni baada ya kuifunga Real Madrid mabao 2-1 katika mechi ya marudiano iliyopigwa kwenye Uwanja wa Santiago Bernabéu, na kumaliza na jumla ya mabao 5-1. Bukayo Saka na Gabriel Martinelli waliifungia Arsenal huku Vinícius Júnior akiipatia Real bao la kufutia machozi. Ushindi huu unaendeleza rekodi bora ya vijana wa Mikel Arteta msimu huu barani Ulaya, na sasa watakutana na Paris Saint-Germain kwenye hatua ya nusu fainali. Arsenal ilifika nusu fainali mara ya kwanza mwaka 2006, kisha ikarudia tena mwaka 2009.

 

Mwaka huu 2025, The Gunners wanarejea katika hatua hiyo wakiwa na matumaini makubwa ya kutinga fainali na kuandika historia mpya ya kutwaa taji lao la kwanza la UEFA Champions League. Huku mabingwa watetezi, Real Madrid wakivuliwa ubingwa wa Ulaya kufuatia kipigo cha jumla cha 5-1 dhidi ya Washika Mitutu, Arsenal kwenye robo fainali, miamba mingine ya soka Ulaya, Bayern Munich ilikuwa ikisukumizwa nje ya michuano hiyo pia, kwa kipigo cha jumla cha mabao 4-3 dhidi ya Inter Milan.

…………………MWISHO……………