Miili 217 ya wahajiri yapatikana Italia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i10768-miili_217_ya_wahajiri_yapatikana_italia
Miili zaidi ya 200 ya wahajiri imepatika katika mabaki ya boti iliyozama katika Bahari ya Mediterranean Aprili mwaka jana 2015.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 07, 2016 14:13 UTC
  • Miili 217 ya wahajiri yapatikana Italia

Miili zaidi ya 200 ya wahajiri imepatika katika mabaki ya boti iliyozama katika Bahari ya Mediterranean Aprili mwaka jana 2015.

Mabaharia na wapiga mbizi wa Kiitalia wamesema wamepata miili 217 ya wahajiri kusini mashariki mwa nchi, yapata kilomita 135 kaskazini mwa Libya. Watafiti wa kimaabara wa jeshi la polisi la Italia kwa ushirikiano na ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa nchi hiyo wamesema tayari wameanzisha uchunguzi ili kubaini asili ya wahajiri hao. Hata hivyo inakisiwa kuwa, aghalabu ya wahajiri hao huenda ni watu wanaotoka barani Afrika kwenda kusaka ajira barani Ulaya na wengine wanaokimbia mapigano mashariki ya Kati.

Hivi karibuni, Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR lilisema kuwa, yumkini watu 700 wameaga dunia baada ya boti zao kuzama katika pwani ya Libya, kusini mwa Italia. Habari ziliarifu kuwa, aghalabu ya wahajiri waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni raia wa nchi za Kiafika kama Somalia, Sudan, Ethiopia na Misri.

Wahajiri karibu laki mbili wameingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean katika mwaka huu pekee huku wengine zaidi ya 2,000 wakifariki dunia kwa kuzama baharini. Mwaka jana pekee, wahajiri 3,770 wanaaminika kufa maji baada ya boti zao kutohimili mawimbi ya bahari.