Trump: Iwapo Marekani itashambuliwa, NATO haitakuja kuiokoa
Rais wa zamani wa Marekani amesema kwamba, haitakidi kuwa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO litaenda kuikoa Marekani iwapo nchi hiyo itakabiliwa na mashambulizi.
Donald Trump ambaye anapania kugombea urais wa Marekani kwa mara nyingine tena kwa tiketi ya chama cha Republican alisema hayo katika mkutano wa kampeni mjini Las Vegas, Nevada na kuongeza kuwa, "Tunalipia NATO, lakini hatustafidi inavyofaa kutoka (shirika hilo la kujihami la Magharibi)."
Trump ametilia shaka Kifungu cha 5 cha Hati ya NATO kinachosema kuwa, iwapo nchi moja mwanachama itashambuliwa, nchi zote nyingine zitalichukulia shambulizi hilo kuwa shambulizi dhidi yao.
Rais wa zamani wa Marekani ameeleza kuwa, "Sipendi kukuambieni haya kuhusu NATO, lakini ikitokea tukahitaji msaada wao, mathalani itokee tushambuliwe, siamini kuwa watakuja (kutuhami)."
Mwanasiasa huyo wa chama cha Republican vile vile amemkosoa vikali Rais Joe Biden wa nchi hiyo kwa kuipa Ukraine misaada ya kijeshi wakati huu ambapo nchi hiyo ya Ulaya ipo katika mapigano na Russia.
"Hatuna silaha za kutosha wenyewe, lakini tunapena zana nyingi kwa wengine," ameongeza Trump. Halikadhalika mwanasiasa huyo amedai kuwa iwapo atachaguliwa kuiongoza tena Marekani, atatatua mzozo wa Moscow na Kiev ndani ya saa 24, sambamba na kurejesha amani katika eneo.
Kadhalika rais huyo wa zamani wa Marekani kwa mara nyingine tena amekiri kwamba nchi hiyo imepoteza ushawishi, nguvu na heshima yake duniani kkutokana na uongozi mbovu wa Biden.