WHO yaonya: Kesi za saratani zitaongezeka kwa 77% kufikia 2050
Shirika la Afya Duniani WHO limetahadharisha kuwa, mzigo wa saratani duniani unaongezeka kwa kiwango cha kuogofya, na kwamba kesi za maradhi hayo hatarishi zinatazamiwa kuongezeka kwa asilimia 77 kufikia mwaka 2050.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Saratani (IARC), ugonjwa huo hatari ulisababisha vifo vya watu milioni 9.7 kati ya wagonjwa milioni 20 waliobainika kuwa nao mwaka 2022.
Takwimu za IARC ambayo ni asasi tanzu ya WHO zinaonesha kuwa, mtu mmoja kati ya kila watu watano anaugua aina moja ya saratani, na kwamba mwanaume mmoja kati ya kila wanaume 9 na mwanamke mmoja kati ya wanawake 12 wanafariki dunia kwa maradhi hayo.
WHO inasema hali si shwari kwani idadi inaongezeka mwaka hadi mwaka na hivyo njia pekee ya kukabiliana na ugonjwa huo ni kuimarisha mbinu za kuubaini mapema, kwani hata visababishi vya saratani navyo vinaongezeka.
Shirika la Afya Duniani linasema saratani haipaswi kusalia adhabu ya kifo wakati huu ambapo kuna kampeni za kudhibiti visababishi kama vile matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe na mlo usio bora.
Kwa mujibu wa taasisi ya IARC, pombe inachangia pakubwa ongezeko la kesi za saratani duniani, na kwamba ilipelekea kusajiliwa wagonjwa wapya 740,000 wa kansa mwaka 2020.
Nchi za China, India, na Vietnam, pamoja na nchi nyingi za kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika zinaonekana kuwa na kesi nyingi za saratani zitokanazo na unywaji wa pombe.