Feb 08, 2024 03:02 UTC
  • Chuo Kikuu cha Harvard cha US kuchunguzwa kwa kuwabagua wanachuo Waislamu

Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani kinakabiliwa na uchunguzi wa serikali, baada ya wanachuo Waislamu na Waarabu katika chuo hicho kuwasilisha faili la kulalamikia vitendo vya dhulma, unyanyasaji, chuki na ubaguzi dhidi yao chuoni hapo.

Shirika la kutetea haki za kiraia la 'Muslim Legal Fund of America' ambalo limewasilisha mashtaka dhidi ya chuo hicho kwa niaba ya wanachuo limesema, wanafunzi Waislamu chuo hapo wanafanyiwa vitendo mbali mbali vya chuki na ubaguzi kwa kuwa tu ama ni Wapalestina, Waislamu, Waarabu au waungaji mkono wa Palestina.

Taasisi hiyo imekikosoa vikali Chuo Kikuu cha Havard kwa kushindwa kuwalinda na kuwadhaminia usalama wanafunzi wake Waislamu na Waarabu, ambao mbali na kushambuliwa, wanafanyiwa vitendo vingine vya chuki na ubaguzi kama kuchapishwa habari zao za siri mitandaoni, kudhalilishwa, kutukanwa na hata kutishiwa.

Shirika hilo la kiraia limesema wanafunzi hao Waislamu na Waarabu hasa Wapalestina baadhi ya nyakati wamekuwa wakifanyiwa vitendo hivyo vya udhalilishaji kwa wao kuvalia tu skafu za Palestina (keffiyeh).

Kinaya ni kwamba, ripoti iliyotolewa mwishoni mwa Februari mwaka jana na Kituo cha Haki za Kibinadamu katika Chuo cha Sheria cha Harvard kwa ushirikiano na Tasisi ya Palestina ya Dhamiri, na kisha kuwasilishwa katika Umoja wa Mataifa ililaani uvamizi wa utawala wa Kizayuni wa Israel huko Palestina ikiutaja kuwa ni "uhalifu wa ubaguzi wa rangi, apartheid."

Chuo Kikuu cha Havard

Wanafunzi Waislamu wa Vyuo Vikuu nchini Marekani na hata katika nchi nyingine za Magharibi wamekuwa wakiandamwa na vitendo vya ubaguzi kwa muda mrefu, lakini vitendo hivyo vilishadidi baada ya kujiri Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ya Wapalestina mnamo Oktoba 7.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu CAIR lilitangaza kuwa, malalamiko ya ubaguzi na matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu yameongezeka nchini humo kwa takriban asilimia 180,  katika robo ya mwisho ya mwaka 2023 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha mwaka uliopita.   

Tags